Robo ya nne yaikosesha ushindi UDSM

UZEMBE wa wachezaji wa UDSM Outsiders kwa kufanya madhambi katika robo ya nne ulichangia timu hiyo kupoteza mchezo dhidi ya Savio kwa pointi 69-65.

Mchezo huo wa Ligi ya Kikapu Dar es Salaam, uliofanyika katika Uwanja wa Donbosco, Upanga, wachezaji Mwalimu Heri na Tryone Edward walifanya madhambi mara nne, jambo lililowafanya wacheze kwa woga wakihofia kufanya mara tano.

Kwa mujibu wa sheria za mchezo wa kikapu, inaelezwa mchezaji anayefanya madhambi mara tano hutolewa ndani ya uwanja.

Baada ya Savio kuona kasi ya UDSM imepungua katika robo ya nne, ilitumia nafasi hiyo kucheza kwa kasi na kupata ushindi wa pointi 27-12.

Kabla ya robo ya nne kufika UDSM ilikuwa inaoongoza kwa pointi 53-44, zilizopatikana katika robo tatu za mwanzo kwa pointi 20-17, 14-14, 19-21.

Katika mchezo huo, Brian Mramba aliongoza kwa kufunga pointi 16 akifuatiwa na Sylvian Yunzu aliyefunga 15.

Kwa upande wa UDSM alikuwa Heri aliyefunga pointi 16 akifuatiwa na Evance Davies na Tryone waliofunga pointi 15 na 13 mtawalia.

Related Posts