Arusha. Mahakama Kuu masijala ya Iringa imemuachia huru baba aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa madai ya kumbaka mtoto wake, ikieleza ushahidi dhidi yake haukuthibitisha shtaka bila shaka.
Katika utetezi wake alioutoa katika mahakama ya chini, baba huyo alidai kesi iliyokuwa ikimkabili ilikuwa ni njama kwa vile hakuwa amelipa mahari kwa wakwe zake.
Mkazi huyo wa Kijiji cha Ngelenge, Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, alidaiwa kumbaka binti yake mwenye umri wa miaka 10, Novemba 15, 2021.
Rufaa hiyo ya jinai namba 17831 ya mwaka 2024, ilitokana na uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Ludewa kwenye kesi ya jinai namba 59 ya mwaka 2021.
Uamuzi huo wa rufaa ulitolewa Septemba 9, 2024 na Jaji Dunstan Ndunguru aliyekuwa akiisikiliza.
Jaji Ndunguru baada ya kupitia hoja za rufaa amesema amebaini shtaka hilo halikuthibitishwa bila kuacha shaka.
Mbele ya mahakama hiyo ya chini, baba huyo alishtakiwa na kutiwa hatiani kwa ubakaji, kosa alilodaiwa kutenda kinyume na kifungu cha 130(1)(2)(e) na 131(1) cha Kanuni ya Adhabu.
Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, ulidai siku ya tukio saa sita usiku, mwathirika wa tukio hilo akiwa amelala na ndugu zake, baba yake aliingia chumbani kwao na kumbaka.
Shahidi wa kwanza ambaye ni mama wa mtoto alidai aliamka na kugundua mumewe hayupo ndani na alipokagua sehemu za siri za binti yake alikuta mbegu za kiume.
Mama huyo alidai baadaye, asubuhi alimuuliza mwathirika kilichotokea usiku uliopita, alidai kuwa baba huyo alikuwa amelala juu yake.
Alidai kesi hiyo iliripotiwa kwa mamlaka ya kijiji na shauri hilo lilitatuliwa lakini baadaye mumewe huyo alikamatwa.
Katika utetezi wake, baba huyo alisema utetezi atakaoutoa ni ule wa kutokuwepo eneo la tukio, kwa tarehe husika iliyotajwa kutendeka kwa tukio.
Katika hoja zake, mshtakiwa alidai siku ya tukio alikuwa akilima shamba eneo la mbugani na alilala hukohuko.
Anadai aliporudi nyumbani siku iliyofuata, aliitwa ofisi ya kijiji na kuarifiwa kuhusu shtaka lililotolewa dhidi yake.
Alijitetea kwamba hakuwahi utenda kosa hilo bali kesi hiyo ni njama dhidi yake kwa sababu hakuwa amelipa mahari kwa wakwe zake.
Hata hivyo, alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Katika rufaa yake, mkazi huyo wa Ludewa aliwasilisha sababu saba ikiwemo ukinzani wa ushahidi wa upande wa mashtaka, kushindwa kuzingatia utetezi wake na ushahidi wa mama wa mtoto kupokelewa kinyume na kifungu cha 127(2) cha Sheria ya Ushahidi.
Pia alidai kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuwaita mashahidi muhimu waliolala na mwathiriwa siku ya tukio na haukuthibitisha shtaka hilo pasipo shaka.
Mkazi huyo aliwasilisha rufaa yake mwenyewe bila msaada wa wakili huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Daniel Lyatuu, ambaye alipinga rufaa hiyo.
Wakili Lyatuu alidai kuwa hakukuwa na ukinzani wa ushahidi kati ya mama na daktari aliyemchunguza mtoto huyo Novemba 16, 2021.
Alisema daktari alithibitisha kutendeka kwa kosa na ushahidi wa Fomu ya Polisi namba tatu (PF3) ulithibitisha kosa hilo kutendeka, ingawa fomu hiyo haikuonyesha uwepo wa mbegu za kiume, hivyo haikuwezekana kufanya uchunguzi wa DNA.
Wakili huyo alieleza kuwa mwathiriwa alitoa ushahidi kuwa hakuwahi kufanya tendo la ndoa kabla ya kubakwa na baba yake na kwamba, hakuna idadi maalumu ya mashahidi wanaohitajika kuthibitisha ukweli.
Pia alisema mwathiriwa alimtambua mrufani kwa kutumia mwanga wa tochi kutoka kwake kwa kuwa hakuwa mgeni kwake.
Katika maelezo yake, mshtakiwa alidai kuwa michubuko kwenye sehemu za siri za mwathiriwa huenda ilisababishwa na vidole vya daktari alipokuwa akimchunguza.
Hivyo, ushahidi huo unapaswa kupuuzwa. Alidai pia kuwa kushindwa kwa upande wa mashtaka kuwaita mashahidi waliolala chumbani na mwathiriwa, ni dosari na ushahidi kuwa mashtaka dhidi yake yanatokana na migogoro ya kifamilia.
Jaji katika hukumu yake ameeleza kuwa atajadili hoja za rufaa dhidi ya ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu.
Amesema kuhusu ukinzani wa ushahidi, kumbukumbu zinaonyesha mama wa mtoto alidai kuwa alipoamka hakumkuta mume wake kitandani.
Mama huyo alieleza kuwa alimuona mumewe akitokea chumba cha watoto na alipohojiwa, alidai kumuona mumewe akishuka kutoka kitandani kwa watoto akiwa amejifunika shuka.
Jaji amesema amebaini kuwa ushahidi wa mama wa mtoto na mwathiriwa unakinzana na kwamba migongano hiyo inaathiri uaminifu wao na inaenda kwenye mzizi wa kesi.
Ameendelea kueleza kuwa hakuna idadi ya mashahidi inayotakiwa kuthibitisha ukweli, lakini kwa kuwa mwathiriwa alikuwa amelala na wenzake wawili, hao wangekuwa wa kwanza kusikia kelele alizopiga mwathiriwa.
Kwa kuzingatia dosari hizo, Jaji ameamua kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kosa hilo bila kuacha shaka yoyote, hivyo ameikubali rufaa na kufuta hukumu ya awali, kisha akaamuru mshitakiwa aachiwe huru isipokuwa kama anashikiliwa kwa kosa lingine.