Dodoma. Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeanza utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambapo Sh72.8 bilioni zitatumika kwenye miradi mbambali kadhaa ikiwemo ya kujenga na kusambaza mifumo ya nishati hiyo.
Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Nishati Mbadala wa REA, Advera Mwijage ameyasema hayo leo Jumatano Septemba 11,2024 wakati akizungumzia kuanza kwa utekezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia uliozinduliwa Mei 2024.
Advera amesema kati ya fedha hizo, Sh35.23 bilioni zitatumika katika ujenzi na usambazaji wa mifumo ya nishati safi kwa Jeshi la Magereza.
Amesema miongoni mwa kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa mifumo 126 ya bayogesi na usimikaji wa mifumo 64 ya gesi miminika (LPG).
“Usimikaji wa mifumo ya gesi asilia mradi mmoja, usambazaji wa mitungi 15,920 ya LPG ya kilo 15 ikiwa na jiko la plate mbili kwa watumishi wa magereza na usambazaji wa tani 865 za mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe kutoka Shirika la Taifa la Madini (Stamico),” amesema.
Advera amesema mradi huo unaotekelezwa kwa miaka mitatu katika magereza 129 yaliyopo Tanzania Bara, utawajengea uwezo watumishi 280 wa jeshi hilo.
Amesema mkataba mwingine utakaosainiwa ni wa Sh5.75 bilioni ambazo zitatumika katika kutekeleza miradi ya ujenzi na usambazaji wa nishati hiyo kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Katika jeshi hilo, itajengwa mitambo ya bayogesi tisa, majiko 291 ya kutumia mkaka mbadala, ujenzi wa mifumo 180 ya kupikia inayotumia LPG na sufuria zake, ununuzi wa tani 110 za mkaa unaotokana na makaa ya mawe pamoja na mashine za kutengenezea mkaa mbadala.
Amesema mradi huo wa miaka miwili, utakaokwenda kutekelezwa katika kambi za 22 zilizopo kwenye mikoa 14, Tanzania Bara, utatoa mafunzo kwa vijana wapatao 50,000 wa JKT.
Aidha, Advera amesema Sh10 bilioni zitatumika katika kuziwezesha kaya za vijijini na zile zilizopo katika maeneo ya vijiji-mji kutumia nishati safi za kupikia zilizoboreshwa.
Amesema mitungi 45, 2445 ya kilo sita (mtungi ukiwa na gesi, kichomeo na mafiga) itasambazwa kwa bei ya ruzuku katika mikopo yote ya Tanzania Bara na kila wilaya itanufaika na mitungi 3,255.
Advera amesema kila mtungi utauzwa kwa bei isiyozidi Sh20, 000 badala ya bei isiyo na ruzuku ya Sh45,000.
Pia amesema kwa upande wa majiko banifu, REA imetenga Sh15 bilioni kwa ajili ya kuwezesha usambazaji wa majiko banifu zaidi ya 200,000 ambayo yatauzwa kwa bei ya ruzuku kwa mikoa yote ya Tanzania bara.
Amesema Sh6.82 bilioni zitatumika katika ufadhili wa mradi wa usambazaji wa gesi asilia wenye lengo la kusambaza gesi asilia na kuimarisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia katika maeneo ya vijijini.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa REA, Martha Chassama amesema lengo la miradi hiyo ni kupunguza changamoto katika misitu nchini, uharibifu wa mazingira na masuala ya afya.
“Madhara ya kutumia nishati chafu ya kupikia ni mengi ikiwemo ukatili wa kijinsia na maradhi mbalimbali,” amesema Martha.