Sintofahamu uchaguzi CUF, Lipumba apata wapinzani

Miaka 32 sasa imepita tangu Chama cha Wananchi (CUF) kilipopata usajili wa kudumu kama chama cha siasa, huku kikipitia milima na mabonde hadi kufikia sasa, kikiwa ni moja kati ya vyama vitano vikubwa nchini.

Chama hiki kimepitia hatua mbalimbali za ukuaji wake, kiliwahi kuwa chama kikuu cha upinzani nchini na chama kilichoshiriki kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya uchaguzi wa mwaka 2010.

Sasa chama hiki kinaelekea kwenye uchaguzi mkuu kikiwa kinakabiliwa na changamoto za kifedha kwa ajili ya maandalizi ya mkutano mkuu utakaokuwa mahsusi kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.

Tayari makada kadhaa wa chama hicho wamejitokeza kuwania nafasi ya uenyekiti taifa, akiwemo Maftah Nachuma, Wilfred Lwakatare, Mneke Jaffar, Hamad Mohamed pamoja na Profesa Lipumba, ambaye inadaiwa amechukuliwa fomu na wafuasi wake.

Wagombea hao waliochukua na kurejesha fomu, wanaeleza sababu za kutaka kukiongoza chama hicho na vipaumbele vyao katika kukijenga na kukiimarisha ili kiwe na mvuto kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Uchaguzi wa viongozi wa CUF uliotarajiwa kufanyika Septemba 15, 2024, umesogezwa mbele hadi Desemba 13, 2024 kwa kile kilichoelezwa kuwa ni changamoto za maandalizi ya mkutao mkuu.

Kinyang’anyiro hicho, kitahusisha nafasi tatu za mwenyekiti, makamu mwenyekiti (Tanzania Bara na Zanzibar) na wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho lililopo kwa mujibu wa katiba yao.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu uchaguzi huo, Naibu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Yusuf Mbungiro anasema dirisha la kuchukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi hizo, pia, limesogezwa mbele hadi Oktoba 30, 2024.

Awali, dirisha la uchukuaji na urejeshaji wa fomu lilifunguliwa Agosti Mosi, 2024 likihusisha nafasi tatu za juu na lilitakiwa kufungwa Agosti 25, 2024, lakini changamoto za maandalizi zimewalazimu kuongeza muda.

“Tumesogeza muda mbele na mkutano wetu mkuu wa kuchagua viongozi utafanyika Desemba 13 hadi 15, 2024. Kwa hiyo, dirisha la kuchukua na kurejesha fomu bado liko wazi pamoja na kuendelea na chaguzi kwa baadhi ya wilaya za kichama ambazo hazikufanya,” anasema Mbungiro.

Anasema sababu nyingine ya kupeleka mbele uchaguzi huo ni kutoa uhuru kwa wilaya 27 za kichama ambazo hazikufanya uchaguzi watekeleze jukumu hilo.

“Wilaya nyingi za kichama zilikuwa zimefanya uchaguzi, lakini zilizobakia ni 27, zinatakiwa zifanye lakini kama hawatafanya kwa muda huo kwa sababu mbalimbali, basi tutaendelea na uchaguzi mkuu,” anasema.

Katika maelezo yake, Mbungiro anadai idadi ya waliochukua na kurejesha fomu ni shughuli aliyowaachia maofisa wake wachakate na ndani ya siku tatu watakuwa wamemkabidhi orodha kamili.

Alipotafutwa kuzungumzia mchakato huo, Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa CUF, Mohamed Ngulangwa alisema idadi ya waliochukua fomu hadi sasa katika nafasi ya mwenyekiti Taifa ni saba, akiwemo mwenyekiti wa sasa, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye alichukuliwa fomu.

“Lipumba amechukuliwa fomu na wanachama wa CUF, baada ya kumuomba na kumbembeleza ndipo alikubali achukuliwe.

“Wanaamini anaweza kuwafikisha mbali kwa kuwa wametoka naye mbali na amekuwa akizunguka wilaya zote kuwatembelea,” anasema Ngulangwa.

Ngulangwa anasema kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara na Zanzibar, pande zote za muungano, watu sita wamejitokeza kila upande.

“Katika idadi hiyo, ni wachache wamerejesha fomu hadi sasa, lakini kwa kuwa muda bado, ngoja tusubiri watakuja kwa kuwa muda bado wanao,” anasema Ngulangwa.

Mmoja wa wagombea wa nafasi ya uenyekiti, Wilfred Lwakatare anaonyesha wasiwasi wa kusogezwa mbele kwa uchaguzi huo kwa kile alichoambiwa kuwa ni changamoto ya fedha za kuitisha mkutano mkuu.

Lwakatare anasema amewashauri viongozi kwamba, wagombea wa nafasi za juu washirikishwe kuhusiana na changamoto hiyo ili wachangie mawazo kuhusu namna ya kupata fedha za kuitisha mkutano mkuu.

“Hiki chama wakati tunakianzisha hatukuwa hata na senti tano, lakini tuliendelea hadi chama kilipofika, tulifika mahali tukapata ruzuku ya Sh160 milioni kwa mwezi, lakini tumeshuka hadi kuwa na Sh25,000 kwenye akaunti, chama chenye usajili namba mbili.

“Hiki chama kina watu, inategemea na ushirikishaji pale unapokwama, ukiwashirikisha vizuri, hakuna mahali unapoweza kukwama. Nakumbuka kuna wakati tulihitaji Sh1 bilioni za kufanya mkutano mkuu. Hiyo hela hatukuwa nayo, lakini ilipatikana kutoka kwa wanachama,” anasema Lwakatare.

Anasisitiza wakutane kushauriana ili mkutano mkuu ufanyike Septemba hii kusudi washiriki uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 wakiwa na safu ya viongozi wapya.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa CUF, Mohamed Ngulangwa, wanachama saba wa CUF wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi ya uenyekiti. Hata hivyo, kwa kuwa muda wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu umesogezwa mbele, hakutaka kuwataja.

Lakini Ngulangwa amethibitisha mmoja wa watu waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo ni mwenyekiti wa sasa, Profesa Lipumba ambaye anasema amechukuliwa fomu na mashabiki zake.

Jitihada za kumpata Profesa Lipumba kwa simu ili kuthibitisha na kueleza sababu za uamuzi wake wa kugombea tena uenyekiti, hazikuweza kufanikiwa.

Profesa Lipumba amekuwa mwenyekiti wa CUF kwa muda mrefu kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2015 alipoandika barua ya kujiuzulu nafasi yake baada ya vyama vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumpitisha Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa kuwa mgombea urais.

Hata hivyo, baada ya miezi michache, alitengua barua yake ya kujiuzulu na kurejea kwenye nafasi yake, jambo ambalo lilisababisha mzozo na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, hayati Maalim Seif Sharif Hamad.

Baada ya kutambuliwa na Mahakama Kuu katika kesi iliyofunguliwa dhidi yake, Machi 2019, Profesa Lipumba alichaguliwa kwa mara nyingine na mkutano mkuu kuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa miaka mitano.

Akizungumza na Mwananchi, kada mkongwe wa chama hicho, Wilfred Lwakatare anasema sababu za kuchukua fomu ni kutaka kuitumikia CUF na kutoa mchango wake ili kukijenga na kukisimamisha kitoe ushindani kama ilivyokuwa zamani.

Hata hivyo, Lwakatare hana hofu kwa wagombea waliojitokeza kuwania nafasi hiyo, akisema ana sifa na uzoefu wa kutosha kushika nafasi ya uenyekiti kutokana na historia yake ya siasa nchini.

Lwakatare amewahi kuwa mbunge wa Bukoba Mjini kwa tiketi ya Chadema kati ya mwaka 2015/2020. Pia, amewahi kuwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema.

Baada ya kuvunjwa kwa Bunge, mwaka 2020, Lwakatare alirejea CUF, chama alichoshiriki kukiasisi wakati wa mageuzi na kukitumikia katika nafasi mbalimbali za uongozi kabla ya kutimkia Chadema.

Hamad Masoud ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, anasema ni haki ya kila mwanachama kugombea nafasi anayotaka ndani ya chama hicho kilichowahi kuvuma miaka ya 2000.

“Kwa kweli hakuna kipya ambacho nitakifanyia chama nikipitishwa, ni pale ambapo viongozi wengine wamefikisha na kazi yangu ni kuhakikisha CUF kinapata ushindi mkubwa katika chaguzi zinazokuja,” anasema.

Kwa mujibu wa Masoud, Katiba ya CUF inasema mwenyekiti akitoka Bara, katibu mkuu atatoka upande wa pili wa muungano, mwenyekiti akitoka Zanzibar, katibu mkuu atatoka upande wa pili wa Muungano, hailazimishi atoke Bara au Visiwani.

Kuhusu ushindani miongoni mwa wagombea, Masoud anasema; “ushindani upo kwa sababu wote ni viongozi, tuna uzoefu, tunajulikana. Kwa hiyo, kila mtu atapimwa kwa mujibu wa mtu anayechagua na kwa sababu zipi.”

Kuhusu kuvaa viatu vya Profesa Lipumba, Masoud anasema wao wanaendeleza alipoishia, kama vilikuwa vikubwa watajitahidi, kwani anaweza kuvaa viatu vinavyomvaa, mwenyeki huyo namba yake ni kubwa.

Masoud aliwahi kuwa Waziri wa Miundombinu katika Serikali ya Umoja Kitaifa (SUK) katika kipindi cha mwaka 2010/15.

Hata hivyo, baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif kutimkia ACT Wazalendo na yeye alimfuata.

Hata hivyo, hakudumu kwa muda mrefu baada ya kushindwa katika uchaguzi wa mwenyekiti wa ACT Wazalendo mwaka 2022, uliomweka madarakani Juma Duni Haji, aliyerithi mikoba ya Maalim Seif.

Mwenyekiti wa CUF, Wilaya ya Newala, Mneke Jaffar anasema ameamua kutumia haki yake ya kikatiba kutia nia ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa CUF Taifa akiwa na dhamira ya kuleta mabadiliko kupitia vipaumbele vyake.

Anasema jambo la kwanza atakalolilifanya akichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CUF Taifa ni kuirejesha kwenye misingi yake.

“Chama hiki kilikuwa na misingi maalumu ya kuwaunganisha Watanzania na kuwatetea. Endapo nitapata ridhaa ya kuwa mwenyekiti wa CUF, nitalisimamia kwanza, pamoja na mambo mengine, ni kuirejesha katika misingi yake ya kuasisiwa,” anasema.

Anasema kipaumbele chake kingine ni kuifanya kuwa chama imara kwa sababu kilikuwa chama kikubwa na kilikuwa kimekaribia kuingia Ikulu, lakini sasa kimeshuka hadhi, kutoka chama kikuu cha upinzani na kuwa chama cha kawaida.

“Moja ya dhamira yangu ni kuirejesha kuwa chama chenye uwezo wa kushindana na kushinda katika chaguzi mbalimbali, ukiwamo wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, kuwa na wabunge wa kutosha na kuongoza halmashauri mbalimbali,” anasema.

Kwa upande wa Zanzibar, anasema walikuwa wamefika nusu ya safari na walikuwa wameingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini sasa hivi wametolewa. Kwa hiyo, anasema anakwenda kuirejesha CUF katika viwango vyake, nguvu yake ya ushindani.

“Tunahitaji uwazi uwepo, kuwe na uwajibikaji wa viongozi, tunahitaji viongozi ambao watatetea wanachama na wananchi kwa ujumla, kutetea haki sawa kwa wana-CUF na hata wale wasio wana-CUF,” anasema.

“Nimejipima na kujiona ninafaa sana kuliko wagombea wengine, akiwemo mwenyekiti wa sasa Profesa Lipumba, ambaye nimejulishwa kwamba naye anataka kugombea. Ninaamini kwamba nitaaminiwa na kuweza kupata ushindi huu,” anasema kada huyo.

Related Posts