Berberati. Kikosi cha saba cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kinachohudumu Jamhuri ya Afrika ya Kati chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa (MINUSCA), kimetunukiwa nishani za umoja huo.
Akizungumza wakati akitunuku nishani hizo jana Septemba 10, 2024, Kamanda wa vikosi vya Umoja wa Mataifa katika ujumbe wa MINUSCA, Luteni Jenerali Humphrey Nyone amesema tangu kikosi hicho kianze jukumu lake katika robo ya mwisho ya mwaka 2023, kimetekeleza majukumu ya ulinzi wa amani kwa weledi.
Amesema kikosi hicho kimehakikisha mazingira salama na tulivu kwa wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambao hivi sasa wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii bila bughudha.
“Na leo ninakabidhi nishani hizi na ninatoa salamu za pongezi kutoka kwa mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ujumbe wa MINUSCA, Valentina Rugwabiza,” amesema Luteni Jenerali Nyone.
Amesema mpaka sasa kikosi hicho kimeendelea pia kuyawezesha mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake kwa urahisi.
Hivyo, amesema nishani hizo zilizotolewa ni uthibitisho wa kutambua mchango mzuri wa kazi inayofanywa na kikosi hicho Afrika ya Kati kwa takribani miezi 10 sasa.
Kwa upande wake, Kamanda wa kikosi hicho, Luteni Kanali Joseph Mushilu amesema: “Tunapoelekea na kukamilisha jukumu letu, tunashukuru kwa ushirikiano wenu na vikosi vingine vinavyotuzunguka.”
Amesema wataendelea kuhakikisha hali ya usalama inaendelea kuwa tulivu.
“Matumaini yangu ni kwamba, jukumu hili litatekelezwa na Kikosi cha nane (TANBAT 08) kwa utimilifu kama ilivyokuwa kwa kikosi cha saba.”
Kamanda huyo pia amesema kwa niaba ya maofisa na askari wa kikosi hicho, wanamshukuru kamanda wa vikosi vya ujumbe wa MINUSCA kwa ushirikiano anaowapatia.
Umoja wa Mataifa hutunuku nishani za heshima kwa walinda amani kila mwaka, kutambua mchango wao katika ulinzi wa amani katika maeneo mbalimbali duniani.
Sherehe hizo zimefanyika makao makuu ya kikosi hicho katika Mtaa wa Greenfield, mjini Berberati na kuhudhuriwa na wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa, viongozi wa serikali na wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.