Dar es Salaam. Ununio ni moja ya maeneo yaliyopo wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, likiwa kaskazini mwa Jiji jirani na Bahari ya Hindi.
Eneo hili lililo jirani na Mbezi Beach na Tegeta linajulikana kwa kuwa na fukwe nzuri na mandhari ya utulivu, likikua kwa kasi katika maendeleo ya miundombinu ya makazi.
Ununio ikiwa moja ya mitaa katika Kata ya Kunduchi ina wakazi 7,469 kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Mwinyijuma Shehe.
Hata hivyo, kama maeneo mengine ya pembezoni mwa jiji, Ununio bado lina maeneo ambayo hayajapimwa vizuri, huku kukiwa na nyumba zilizokamilika ujenzi lakini hazikaliwi na watu, zingine zikiwa hazijakamilika ujenzi.
Waswahili husema, uzuri wa mkakasi ndani kipande cha mti. Ndani ya Ununio, eneo la Kwa Wasomali linatia doa mandhari hii.
Kwa Wasomali ni eneo linaloogofya hususani usiku likiwa na simulizi za kusikitisha za matukio ya uhalifu na mauaji.
Eneo hilo lina msitu wenye miti minene na vichaka, baadhi ya wahalifu wakilitumia kwa maficho yao. Msitu huu umepakana na makaburi na mashamba ya chumvi.
Ndani ya msitu huu kwa mujibu wa wananchi waliozungumza na Mwananchi baadhi ya wahalifu huutumia kutekeleza mauaji au kutupa miili ya watu waliouawa.
Kwa mujibu wa wananchi, msitu huo unatumika na magenge ya kihalifu kutoka maeneo mbalimbali nje na Ununio.
Ukubwa wa eneo la msitu la takribani kilomita mbili na umbali wake kutoka kwenye makazi ya watu ni moja ya sababu ya kuwa maficho ya wahalifu.
Wakazi wa Ununio hupata huduma kutoka vituo vya polisi vya Tegeta, Mbweni na Kawe ambavyo kwa mujibu wa wakazi vipo umbali wa zaidi ya kilomita tano.
Februari 11, 2018 kiongozi wa Chadema, Daniel John alitekwa na kisha aliuawa wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni. Mwili wake ulipatikana Februari 14, mwaka huo kwenye msitu huo.
Msanii wa miondoko ya Hip Hop, Ibrahimu Mussa maarufu Roma Mkatoliki, Aprili 2017 baada ya kutekwa alieleza alitelekezwa Ununio.
Mbali ya matukio hayo, katika siku za hivi karibuni yameelezwa mengine ya aina hiyo kutokea.
Kwa mujibu wa wakazi wa Ununio wamewahi kuripoti matukio ya miili kupatikana katika msitu huo au karibu na maeneo ya makaburi, hali iliyowafanya wengi waogope kukaribia eneo hilo, hasa usiku.
Tukio la hivi karibuni ni la kada wa Chadema, Ally Kibao aliyetekwa na watu wasiojulikana jioni ya Septemba 6, 2024, eneo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar es Salaam akiwa ndani ya basi la Tashriff akielekea nyumbani kwake, mkoani Tanga.
Mwili wa Kibao ulikutwa Ununio, Dar es Salaam na ulizikwa Jumatatu Septemba 9, katika Kijiji cha Tarigube Kata ya Togoni, mkoani Tanga.
Akizungumza na Mwananchi Septemba 10, 2024 Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ununio, Mwinyijuma Shehe anasema katika kipindi cha hivi karibuni wameshaokota maiti nne zikiwa zimetelekezwa, mwanamke mmoja na wanaume watatu.
“Kipindi cha miaka minne nyuma tulikuwa tunaokota maiti tatu hadi nne kwa wiki. Nilikuwa nikipigiwa simu na wananchi, Mwenyekiti kuna mtu huku amefariki tukifika eneo la tukio tunatoa taarifa kwa Jeshi la Polisi wakifika wanachukua mwili,” anasema.
Anasema baadhi zilizookotwa zilisafirishwa na maji ya bahari zikiwa za watu waliokuwa wakiogelea au wavuvi.
Shehe anasema matukio yanayoendelea yanawaogofya wananchi hata kama si wakazi wa Ununio kwa historia inayowekwa.
Kwa mujibu wa Shehe, baadhi ya wakazi wa Mbweni inawalazimu kuzunguka Tegeta ili kufika makwao badala ya kupita Ununio.
Wananchi wameeleza wamekuwa wakifanya mikutano ya mara kwa mara kati ya viongozi wa jamii na maofisa wa polisi wa Mbweni, Mbezi Beach na Tegeta kupanga mikakati ya kudhibiti uhalifu.
Shehe anasema walikaa vikao ili atafutwe mmiliki wa eneo lenye msitu huo ambako pia kuna magofu aweze kulifanyia usafi.
“Si tu kutafutwa muhusika lakini pia tumependekeza kuwepo doria za mara kwa mara, hasa usiku kwenye maeneo ya msitu huo na sehemu zingine zinazotajwa kuwa hatari, hii itasaidia wahalifu kuogopa,” anasema.
Anasema eneo hilo lililo jirani na barabara linapaswa kuwekwa taa.
Gervas Mkude, mkazi wa eneo hilo anasema kunahitajika ulinzi wa polisi kusaidia kulinda usalama wa eneo hilo kwani ulinzi shirikishi ni ngumu kufanyakazi eneo hilo.
“Tunapoona magari yamesimama tunashindwa kuhoji kwa sababu hujui unayemuhoji ni nani, hivyo tunapita na mambo yetu lakini polisi ana uwezo wa kuhoji na akapatiwa majibu,” anasema Mkude.
Anadai hata siku ambayo mwili wa Kibao ulipatikana kuna gari lilisimama eneo hilo kwa takribani dakika 45 na baada ya kuondoka ndipo ulipoonekana mwili huo.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule anasema mazingira ya eneo la Kwa Wasomali yanayolalamikiwa kwa sasa hawana utaratibu wa kubomoa nyumba zilizopo au kukata miti iliyopo.
“Jana (Septemba 10) nilipita kukagua, kuna mikoko na ni miti ambayo si rahisi kuikata na hakuna msitu mkubwa wa kusema wahalifu wanakaa hapa ila usafi tutaendelea nao, siyo hapa tu kwani kuna maeneo mengine pia kama ya Oysterbay, Mbezi Beach na hata Salasala kuna vichaka ambavyo tunatakiwa kuviondoa,” anasema Mtambule ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.
Anasema ametoa maagizo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha ulinzi shirikishi unafanya kazi ya hali ya juu kwa mujibu wa sheria.
Ameagiza eneo ambako hakuna ulinzi shirikishi uanzishwe haraka na unakolegalega uimarishwe.
“Niwatoe hofu wakazi wa Ununio wa eneo la Kwa Wasomali hatuna kitisho cha usalama ni tukio tu limetokea na Serikali inaendelea kulifanyia kazi kwa maana ya uchunguzi na hatua zitachukuliwa,” amesema.
Kwa wakazi wote wa Wilaya ya Kinondoni, amesema kila mmoja ashiriki kwenye ulinzi shirikishi ikiwa ni pamoja na kuteua vijana waliopata mafunzo ya mgambo na waliokaguliwa na Jeshi la Polisi.
Anasema mhalifu hawezi kwenda katika eneo hilo kama ulinzi umeimarishwa.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro anasema katika eneo la Kwa Wasomali wahusika wanaomiliki eneo hilo wanatakiwa kufanya usafi wa mazingira kwa kuondoa miti iliyopo.
“Wahusika wa eneo hilo wanatakiwa kukata miti iliyopo kama kilichofanyika daraja la Selander na hatimaye sasa kuna usalama wa kutosha na kunatakiwa kuwepo taa,” anasema Muliro.
Ametoa wito kwa wakazi wa Ununio wawe na ulinzi shirikishi kwani hakuna mtu atakayewalindia eneo lao kama wao wenyewe hawajawa na ulinzi shirikishi.
Amesema Jeshi la Polisi kwa sasa linaendelea kuimarisha ulinzi na kufanya intelijensia kuwakamata wahusika na kuliangalia kwa karibu eneo hilo.