Unguja. Ili kufahamu hali ya soko la ajira, upungufu wa ujuzi unaohitajika siku za baadaye Serikali inakusudia kufanya utafiti maalumu kupitia mradi wa Sebep.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff amesema hayo alipojibu swali la mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi.
Akijenga swali lake, Ameir amesema tafiti zinaonyesha kuwa katika uchumi wa Afrika vijana watatu kati ya wanne hawana ujuzi wa kushiriki katika uchumi wa kidijitali wa Afrika.
Ametaka kujua mikakati iliyopo ya kuona vijana wanakuwa katika sehemu kubwa ya uchumi huo.
Akijibu swali hilo leo Septemba 11, Waziri Shariff amesema Serikali inakusudia kufanya utafiti maalumu hivi karibuni kufahamu hali ya soko la ajira kwa kina nchini.
“Jambo ambalo litaonyesha hali ya fursa zilizopo, ujuzi uliopo, upungufu wa ujuzi na ujuzi utakaohitajika siku za baadaye, ili Serikali iendelee kuchukua hatua stahiki za ukuzaji ujuzi, ambazo zitasaidia katika kuimarisha vyuo vyetu kwa kuweka mitalaa inayoendana na hali halisi ya soko la ajira,” amesema.
Amesema wizara kupitia idara ya ajira imekuwa na programu kadhaa, zikiwamo za kutambua ujuzi na uzoefu wao wa kazi wakiwa hawana vyeti vya masomo ya kazi husika, mafunzo kazini baada ya masomo, kukuza ujuzi hasa kwa vijana ili waweze kujiajiri na kuajiriwa.
Waziri amesema suala la matumizi ya kidijitali katika kukuza uchumi nalo linashughulikiwa.