Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Jenister Mhagama ameahidi kukamilisha haraka mchakato wa Bima ya Afya kwa Wote, ambao kwa sasa upo katika hatua ya kuandaa kanuni.
Desemba 4, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alitia saini muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kuwa sheria kamili.
Akizungumza leo Septemba 11, 2024, baada ya kutembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Waziri Mhagama amesema gharama kubwa za matibabu zinawakabili wananchi na Bima ya Afya kwa Wote ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya.
“Tangu nimeanza ziara jana, hoja kubwa ni gharama za matibabu. Lazima maswali ya wananchi tuyapatie majibu na Bima ya Afya kwa Wote ndiyo itakayomsaidia kila Mtanzania kupata huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa,” amesema Waziri Mhagama.
Katika ziara yake, ametembelea pia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na Ubongo Muhimbili (MOI) pamoja na Hospitali ya Mloganzila.
Baadhi ya wagonjwa wameeleza jinsi walivyolazimika kuuza mali zao ili kugharamia matibabu.
Jafari Malingizi, ndugu wa mgonjwa aliyelazwa MOI, amesema mtoto wake alifanyiwa upasuaji wa kichwa kwa gharama ya Sh2.6 milioni, baada ya kupata ajali ya pikipiki na kulazimika kuuza mali zake kumgharimia.
“Nililazimika kuuza pikipiki, magunia ya mahindi na mbuzi ili kugharamia matibabu,” alisema.
Rajabu Sabani, kwa upande wake, amesema mama yake alifanyiwa upasuaji wa kichwa, na ametumia zaidi ya Sh3 milioni.
Amesisitiza kuwa bima za afya hazikidhi gharama za matibabu na aliiomba Serikali kuangalia upya suala hilo.
Edna Ndera, mama mkubwa wa mtoto Ally Mwandi aliyelazwa JKCI, amesema gharama za matibabu ya upasuaji wa moyo ni kubwa. “Matibabu yao ni mazuri, lakini gharama ni kubwa. Ikiwezekana wafanyie maboresho bima ya afya kwani ina ukomo wa matibabu,” alisema.
Kaimu Mkurugenzi wa MOI, Dk Lemeri Mchome, amesema wanatekeleza sera ya uchangiaji gharama, huku akisisitiza kuwa gharama za matibabu katika taasisi hiyo bado ni nafuu ukilinganisha na hospitali binafsi.
“Gharama za upasuaji wa kichwa hapa ni Sh600, 000 wakati hospitali binafsi ni Sh23 milioni. Kwa kawaida kitanda kinagharimu Sh500, 000, lakini mgonjwa analipa Sh80, 000 kwa ICU,” amesema Dk Mchome.
Mkurugenzi wa JKCI, Dk Peter Kisenge, amesema wagonjwa wengi wanaridhika na huduma zinazotolewa kutokana na uwekezaji wa Serikali katika rasilimali watu na vifaa. “Huduma tunazotoa hapa zinafanana na zile za India. Tutaendelea kuimarisha teknolojia ili kuwafikia wananchi waliopo sehemu mbalimbali,” amesema Dk Kisenge.