WAZIRI MKUU AMTAKA MWANAFUNZI ARJUN MITTAL KUONGEZA WIGO UTOAJI TAULO ZA KIKE

 

Na Mwandishi wetu, Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemtaka Mwanafunzi Arjun Kaur Mittal mwenye umri wa miaka 16 kuongeza wigo wa kugawa Taulo za kike kwa wanafunzi nchini.

Arjun Mittal kupitia programu aliyoanzisha ya HERNEEDS ameweza kukusanya fedha zaidi ya Dola 60,000 zilizomwezesha  kununulia  Taulo za kike zaidi ya elfu10 na kuzigawa kwa wanafunzi katika Sekondari 33 zilizopo Arusha.

Akizungumza na Mwanafunzi huyo mtanzania anayesoma Dubai katika Falme za Kiarabu (UAE), katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma hivi karibuni ,Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali Iko tayari kushirikiana nae kufanikisha lengo hilo.

Amempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na umri wake mdogo na kutoa wito kwa wanafunzi wengine kuiga mfano huo ili kusaidia wanafunzi ambao wamekuwa wakikosa masomo kwa siku kadhaa kila mwezi kwa kukosa Taulo za kike.

“Wewe ni Binti mdogo lakini umeweza kufanya mambo makubwa sana, nakupongeza, kama utaweza nakukaribisha jimboni kwangu Ruangwa na maeneo mengine uje utembelee shule na kugawa Taulo za kike na kama Kuna msaada utahitaji Mimi nitakupatia,” amesema Waziri Mkuu.

Arjun amesema amepokea wazo la Waziri Mkuu na kwamba akiwa Dubai atajaribu kuongea na wanafunzi wenzake ili waweze kushirikiana kutafuta fedha za kununulia Taulo za kike na kuja nchini kuzigawa.

Amesema peke yake hatoweza kugawa Taulo za kike kwa kuwafikia maelfu ya wanafunzi lakini akipata watu wa kushirikiana nao ataweza kufanikisha jambo hilo.

” Wanafunzi wengi nchini wamekuwa wakikosa masomo kwa siku kadhaa kila mwezi kutokana na kukosa Taulo za kike, kupitia programu ya HERNEEDS nitajitahidi kuwafikia wengi kwa kadiri nitakavyoweza,”amesema Arjun.

Awali Mwanafunzi huyo aliyekuwa ameongozana na Baba yake Atul Mittal akiwa ofisini kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Bungeni Jijini Dodoma , Dkt Tulia Ackson alimuomba kusaidia kuondolewa kwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye Taulo za kike ili kuzifanya ziweze kuuzwa kwa bei ya chini na kila Mwanafunzi aweze kumudu gharama yake.

 

Related Posts