‘Beach boys’ katikati ya biashara ya dawa za kulevya

Dar/mikoani. Katika maeneo ya pwani ya Tanzania, hasa yenye shughuli za utalii kama Zanzibar, Dar es Salaam na Bagamoyo, kuna kundi maalumu la vijana wanaojulikana kama ‘beach boys’ wanaofanya kazi ufukweni.

Vijana hao hufanya shughuli mbalimbali, ikiwemo kukaribisha watalii na kuwaongoza sehemu mbalimbali za burudani, kuwafundisha watu kuogelea na hata kuwasaidia watalii kuelewa tamaduni za wenyeji.

Wengi hufanya kazi za kuongoza watalii, kuuza bidhaa za utamaduni na wengine hupiga mbizi wakitangaza bidhaa na hata kuburudisha wageni.

Waswahili husema hakuna kizuri kinachokosa kasoro. Baadhi ya vijana hao wamebainika kujihusisha na matukio ya jinai, ikiwamo biashara ya magendo na dawa za kulevya.

Baadhi yao wameshafikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka kuhusu kujihusisha kwao na dawa za kulevya.

Simulizi ya ‘beach boy’

“Nimekuwa ‘beach boy’ kwa miaka zaidi ya 10, awali nilianza kama muongoza watalii, nikionyesha wageni sehemu za kitalii na kuwapangia safari za kwenda visiwani kama vile Mbudya au safari za kupiga mbizi,” anasimulia kijana aliyeacha kazi hiyo aliyeomba kutotajwa jina.

Akizungumza na Mwananchi Agosti 24, 2024 anasema, “kazi ilikuwa nzuri mwanzoni, lakini hivi karibuni wateja walipungua na baadhi ni kutokana na kuogopa.”

Woga wa wateja anasema ulitokana na baadhi yao kujishughulisha na kazi nyingine zenye viashiria vya jinai.

Ni mtazamo wake kwamba, baadhi ya vijana hao huingia kwenye vishawishi vya kutenda makosa ya jinai kutokana na kusaka fedha za haraka ikizingatiwa kuwa wengi wao wanatoka familia duni.

Akieleza jinsi alivyojitosa kwenye kazi hiyo, anasema “nilifundishwa na rafiki yangu, John baada ya kufika ufukwe wa Coco nilikokuwa nikijifunza kuimba.”

Kijana huyo mwenye miaka 32 anasema alipokuwa akijifunza kuimba rafiki yake alimweleza anapaza sauti, hivyo asingefanikiwa kutimiza malengo yake na akamshauri kubadili mwelekeo na kujihusisha na shughuli za majini.

Anasema alikubaliana na rafiki yake ambaye alimkutanisha na watu wengine.

“Nilikutanishwa na watu walioitwa wakuu katika fukwe za bahari, kila eneo lilikuwa na kiongozi wake kuanzia Coco, Ununio, Kunduchi, Mbezi Beach, Feri, Kurasini na Kigamboni,” anasema.

Mbele ya wakuu hao, anaeleza alikula kiapo cha utii na kuficha siri kwa atakayoyaona, akitishwa kwamba endapo atazungumza basi angeuawa na mwili kutoswa baharini.

“Baada ya kula kiapo nikapewa jaribio la kwanza la kubeba kopo ambalo sikutakiwa kulifungua hadi nitakapofika sehemu niliyoambiwa na kumpatia mzigo, mtu ambaye atanipa pesa, huku kukiwa na mtu anayenifuatilia,” anasema.

Kwa kuwa alishakula kiapo, anasema alifanikisha kazi aliyotumwa na aliporejea alikabidhiwa Sh150,000 zilizomfanya aone hiyo ndiyo kazi nyepesi itakayompatia kipato pasipo kujua kopo alilobeba ndani lilikuwa na kitu gani.

Anaeleza alifundishwa kuogelea, huku akiendelea kupeleka mizigo kule alikoelekezwa.

“Nilijifunza kwa mwezi mmoja nikafahamu kucheza kwenye maji na wakati mwingine nilikuwa naingia kwenye boti kuwapeleka watu visiwani, kikiwemo cha Mbudya,” anasemana kuongeza kuwa baadaye alibaini alichokuwa akisafirisha kilikuwa dawa za kulevya.

“Walionituma walikuwa wakitumia simu yangu ndogo nikiwa na laini zaidi ya 10 nikilazimika kuzibadilisha kutokana na kazi niliyokuwa nafanya,” anaeleza.

Kijana huyo anaeleza wamekuwa wakiwafundisha watu kuogelea na usiku ndipo huenda kina kirefu cha maji kwa ajili ya biashara ya dawa za kulevya.

“Wapo wageni kutoka mataifa mbalimbali wanakuwa wanahitaji bangi, kokeini na heroini. Mara ya kwanza niliogopa, baada ya kuona wengine wanachofanya na wanaishi tu vizuri nami nilijitosa,” anasema.

Anasema dawa huingia kwa njia ya boti na wakati mwingine kupitia mizigo kwenye bandari kuu, lakini wao hutumia njia za panya kuzisambaza.

“Mizigo inapofika tulikuwa tunaifuata tukijifanya wavuvi.  Muda ambao tunajua hakuna doria ya askari maji, ulitusaidia kuingia sehemu tunazotaka kufikisha mzigo,” anasema na kuongeza kuwa walikuwa wakikutana na wahitaji wa dawa hizo usiku baharini.

Katika ufukwe wa Bagamoyo, anaeleza kuna wakati walitumia madumu ambayo watu waliowaona walihisi kuwa ni mafuta ya kupikia.

“Kama kulihitajika kushusha mizigo bandarini tulikuwa tunakwenda Bagamoyo yanatupwa madumu, wengi walijua ni mafuta, lakini kati ya madumu 20 unaweza kukuta manane yamejaa mafuta mengine yanachanganywa,” anaeleza.

Anaeleza katika baadhi ya maeneo waliwatumia mabinti wenye watoto kupeleka mizigo kwa wahusika wakijifanya ombaomba.

“Wanawake wenye watoto waliaminika, walijifanya ombaomba na wakati mwingine tuliwapatia wahusika mtoto kumpakata kisha kuchukua kilicho cha kwao ndani ya nepi aliyovaa,” anaeleza.

Anasema alijikuta akitumia kila aina ya mbinu kufikisha mzigo kutokana na vitisho kutoka kwa mabosi wao endapo atashidwa kuwasilisha kile alichotumwa.

“Kuna siku askari polisi walikuwa doria katika baadhi ya maeneo, siku hiyo nilikuwa na mzigo nilijifanya chizi na kuanza kuokota makopo, nikiongea ovyo na kuwaangalia wengine wakiwa wamekamatwa,” anasema.

Anasema aliona maisha yake yakiwa yanaishia gerezani, hivyo hakuwa na namna ya kufanya zaidi ya kufanya hivyo na akaokoka na ikawa ndio mwisho wa kufanya biashara hiyo.

Akizungumza na Mwananchi Septemba 6, 2024, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo anasema wameanza kutoa elimu kwa watu wanaofanya shughuli kwenye fukwe za bahari, wakiwamo wavuvi, wafanyabiashara na beach boys.

“Kwa kushirikiana na wenzetu wa Marine (kikosi cha polisi cha wanamaji) tunawaeleza kile tulichokusudia kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya,” anasema.

Lyimo anasema wanatoa elimu ili wajiepushe na biashara hiyo, iwe kwa kutumia au kusafirisha kwa njia ya maji akieleza wapo wanaofanya hivyo si kwa matakwa yao.

Anasema baada ya elimu inayoendelea kutolewa mwezi huu wa Septemba, wataanza operesheni kuwakamata wote wanaojihusisha na biashara hiyo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

“Tukimaliza kutoa elimu tunaanza kupita kila sehemu kwa ajii ya ufuatiliaji na hapo tukimkamata mtu hatutasikiliza utetezi. Tutakuwa tumetoa elimu ya kutosha na tunajua vijana wengi wanaojihusisha katika maeneo ya bahari ni wale wanaotoka katika familia za hali ya chini,” anasema.

Lyimo anasema wanatambua wapo wanaotembeza watalii, ambao amewaonya wasitumie kigezo hicho kufanya mambo mengine kinyume cha sheria.

“Ili kukabiliana na biashara hii nimeingia mwenyewe kazini kwa kupita sehemu ambazo zimekuwa zikipitishwa dawa za kulevya, ikiwemo mipakani. Nitoe onyo kwa watumishi wanaohusika na maeneo haya hatufanyi mchezo. Tukikamata gari ajue aliyekuwa zamu na yeye tunamkamata,” anasema.

Lyimo anasema utoaji elimu hautaishia kwa wanaojishughulisha baharini pekee, bali pia utahusisha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra), wamiliki wa mabasi na malori, madereva na makondakta wa masafa marefu.

Kamanda wa Kikosi cha Polisi Wanamaji, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Moshi Sokoro anasema kwa kushirikiana na Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wamekuwa wakifanya operesheni kubwa.

Akizungumza hayo Septemba 6, 2024, anasema hivi karibuni watu zaidi ya 60 wamekamatwa kwa makosa ya jinai.

“Operesheni za pamoja zinafanyika, pia tunatoa elimu hata juzi (Septemba 3) nilikuwa Feri tumeliongelea hilo pamoja na uongozi wa Feri, wao wanakiri uvutaji bangi na wengine wanakuja wakiwa wameshavuta dawa zenye kemikali,” anasema.

Anasema uongozi wa Feri umeendelea kuwapa ushirikiano kuona namna wanavyoweza kuliondoa tatizo hilo kama si kulipunguza.

Kwa upande wa masafa marefu, anasema wanashirikana na DCEA kulingana na taarifa za kiintelijensia ambazo huzifanyia kazi kwa kufanya operesheni ya kuzuia na ukamataji wa watuhumiwa.

Related Posts