Dar es Salaam. Kilo 15 za dhahabu yenye thamani ya Sh3.4 bilioni zimekamatwa katika Bandari ya Dar es Salaam ikitoroshwa kwenda Zanzibar.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde Septemba 11, 2024 jijini Dar es Salaam alipozungumza na na vyombo vya habari.
“Nchi yetu inazo sekta kadhaa za uzalishaji ambazo mapato yake ndiyo msingi wa maendeleo ya uchumi wetu ikiwemo sekta ya madini. Sasa basi, tunapokuwa na watu wachache ambao wanajihusisha na shughuli hizi za utoroshaji wa madini na hivyo kuikosesha Serikali mapato hatuwezi kuwavumilia.”
“Kilo hizo 15.78 kwa bei ya leo zina thamani ya takribani bilioni 3.4, fedha ambazo kwa sasa zote watoroshaji hawa wanakwenda kuzipoteza. Serikali tunakwenda kufuta leseni zao wakitiwa hatiani na mahakama na kuwaweka kwenye orodha, ambayo hawataruhusiwa kumiliki leseni ya kufanya biashara yeyote katika mnyororo wa thamani wa madini Tanzania,” amesema Mavunde.
Kwa kwa mujibu wa mahojiano ya awali wakati uchunguzi unaendelea, watuhumiwa wamesema madini hayo walikuwa wanasafirisha kutoka Dar es Salaam kuelekea Zanzibar.
“Uchunguzi na mahojiano na watuhumiwa yanaendelea na pindi kazi hii ikikamilika tutawapandisha mahakamani kujibu mashtaka,” amesema Mavunde.
Mavunde ameipongeza kazi inayofanywa na Kikosi kazi cha kuzuia utoroshaji wa madini kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama na kutoa rai kwa wafanyabiashara nchini kuacha hiyo.