KOCHA wa Pamba Jiji, Goran Kopunovic hajaonja ushindi hata mmoja katika Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini ametamba kwa namna alivyokiandaa kikosi hicho, anaamini kabisa ataanza kuvuna pointi tatu za kwanza keshokutwa Jumamosi dhidi ya Azam FC, akisema wala hana presha na matokeo yaliyopita.
Pamba iliyopanda Ligi Kuu msimu huu sambamba na KenGold ya Mbeya, imevuna pointi mbili tu hadi sasa katika mechi mbili za kwanza za ligi hiyo ikitoka suluhu dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji, lakini kocha Goran alisema hana presha ya matokeo hayo kwani anaamini atapata matokeo mazuri ugenini.
Goran aliyewahi kuzinoa Simba na Tabora United, aliliambia Mwanaspoti anaamini kwa sasa kikosi hicho kimeimarika na kesho itaikabili Azam kwa lengo la kubeba pointi zote tatu ugenini kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Awali mechi hiyo ilipangwa kupigwa leo Ijumaa kabla ya Bodi ya Ligi kuihamishia kesho kuanzia saa 1:00 usiku.
“Naiheshimu sana Azam, hasa baada ya mabadiliko katika benchi lao la ufundi,” alisema Goran akimaanisha ujio wa kocha mpya, Rachid Taoussi atakayeiongoza timu hiyo kwa mara ya kwanza dhidi ya Pamba.
Goran amekiri kuna changamoto za wachezaji wapya, ambao baadhi hawajawahi kucheza mechi za usiku, lakini bado ana imani na uwezo wa timu hiyo kupata matokeo mazuri ikiwa ugenini, licha ya kwamba timu hiyo haijafunga bao katika michezo miwili ya kwanza.
“Tunajitahidi kuboresha uwezo wa kumalizia nafasi tunazozitengeneza na naamini mabao yataanza kuja hivi karibuni,” alisema Goran ambaye anakabiliana na Azam ambayo nayo inajitafuta baada ya kuanza msimu kwa suluhu mbele ya JKT Tanzania na kutolewa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Azam iling’olewa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya awali kushinda nyumbani kwa bao 1-0 kisha kulala ugenini 2-0 kabla ya kutoka suluhu na JKT mechi iliyochezwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo iliyoondoka na kocha Youssouf Dabo aliyeachishwa kazi na kuajiriwa Taoussi kutoka Morocco.
Katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara, leo Ijumaa inapigwa mchezo mmoja tu kwa Wagosi wa Kaya, Coastal Union itakayoikaribisha Mashujaa kwenye Uwanja wa KMC Complex, inayoutumia baada ya Mkwakwani kufungiwa kwa sasa ili kukarabatiwa.
Mashujaa iliyocheza mechi mbili na kushinda mchezo mmoja na mwingine kutoka suluhu, ikiwa na pointi nne inakutana na Coastal iliyoanza msimu kwa sare ya 1-1 dhidi ya KMC, huku kila upande ukitamba kuibuka na ushindi katika mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 10:00 jioni.
Kocha Joseph Lazaro alisema anatarajia ugumu kutoka kwa mpinzani wake kutokana na kukutana msimu wa pili sasa na mifumo yao inafanana na timu hiyo imekuwa ikimpa shida amekiandaa kikosi chake kwa ubora.
“Tunatambua ubora wa Mashujaa ambayo imekuwa ikitupa shida kila tunapokutana nayo hatuwezi kuruidia makosa tumejiandaa kwa ajili ya kupata matokeo ambayo yatatuweka kwenye nafasi nzuri hadi mwisho wa msimu tukihitaji nafasi nne bora,” alisema Lazaro. huku kocha wa Mashujaa, Mohamed Abdallah ‘Bares’, amesema anatarajia mchezo bora na wa ushindani ambao kwa upande wake anaamini atapata pointi tatu kutokana na kufanyia kazi mapungufu aliyoyaona mchezo uliopita.
“Hautokuwa rahisi kutokana na mpinzani wangu kutoka kujeruhiwa, hivyo atakuja na nguvu ili kusaka matokeo mazuri lakini mimi pia nimetoka kuambulia pointi moja dhidi ya Tanzania Prisons, sitakubali kuangusha pointi nyingine hivyo dakika 90 zitaamua ubora.”