HAKIELIMU YAZINDUA MRADI WA MAJARIBIO KUWEZESHA WALIMU KUFUNDISHA KWA VITENDO

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

SHIRIKA la HakiElimu Tanzania limezindua mradi wa majaribio ambao umelenga kukuza ufundishaji wa walimu,kupitia teknolojia ambayo itamwezesha Mwanafunzi kupata picha halisi ya kitu anachofundishwa.

Akizungumza leo Septemba 12,2024 Jijini Dar es salaam Mkuu wa Programu Shirika la HakiElimu Bw.Godfrey Boniventura wakati wa uzinduzi wa mradi huo amesema kuwa mradi huo umekusudia kumfundisha mwanafunzi kwa vitendo na sio nadharia pekee ambapo wanafunzi watafundishwa kwa kutumia vitu katika picha na maumbo yake halisi.

“Hata kama unataka kumfundisha mtu awe makenika (fundi wa gari) labda kufunga mguu wa gari(shock up) unamfundisha kwa maumbo halisi na kumuonesha inapofungwa ambapo anapata picha halisi kwa namna ya kufanya”. Amesema.

Aidha Boniventura amesema baada ya mradi huo wa majaribio kukamilika wanatarajia kutanua wigo kwa kushirikisha taasisi mbalimbali za elimu nchini.

Aidha Boniventura amesema Taasisi ya Hamk ,Save the Children na taasisi 5 za kitaaluma zimeshiriki katika kuhakikisha utekelezaji mzuri wa mradi huo wa majaribio ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ambapo itakuwa njia nzuri ya kupima ufanisi na umuhimu wake katika mazingira ya Kitanzania.

Kwa upande wake kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Dkt. Abdalah Ngodu ametoa shukrani zake kwa waandaaji wa mradi huo ambapo anatarajia kuona ubunifu na mipango yenye matokeo kwenye maisha ya wanafunzi kwa kuzalisha ujuzi wenye kuleta tija kwa jamii.

Aidha amesema kuwa ukuaji wa kasi wa teknolojia,unachangia uhitaji wa zana za kisasa kama teknolojia ya VR na XR ambao pia ni sehemu ya maudhui ya mradi huo ambapo inatoa mwanya kwa wakufunzi na wanafunzi kujifunza mtandaoni kwa pamoja kabla ya kufanya vitendo katika ulimwengu halisi.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali (VTA), Dkt. Bakari Ali Silima amesema uingizwaji wa mfumo wa kidijitali wa maudhui ya mafunzo katika teknolojia ya vipimo vitatu na matumizi ya miundombinu ya TEHAMA, kutawezesha kutumia mwalimu mmoja kutoa mafunzo kwa wanafunzi wengi katika maeneo tofauti kwa wakati mmoja.

Mradi huo wa majaribio unatarajiwa kufanyika kwa miaka miwili ambapo umefadhiliwa na kampuni ya 3D BEAR na kuratibiwa nchini na Chuo kikuu Cha Hamk,Shirika la Save The Children,HakiElimu pamoja na vyuo vikuu Vitano.












Related Posts