Hali ya uvuvi, biashara baada ya ziwa Tanganyika kufunguliwa

Mei 15, 2024 Serikali ya Tanzania ilifunga ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu, ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano na nchi zinazolizunguka ziwa hilo, ikiwemo Zambia, DR Congo na Burundi, lengo lilikuwa ni kufanya utambuzi wa zana haramu za uvuvi na kuruhusu ongezeko la samaki.

Ziwa hilo, ambalo kwa Tanzania lipo upande wa Kigoma, Rukwa na Katavi lilifunguliwa Agosti 15, 2024 na kila mwaka litafungwa kwa miezi mitatu kulingana na makubaliano ya mataifa hayo manne.

Wavuvi ziwa Tanganyika wakitoa nyavu zao kwenye boti baada ya kutoka ziwani

Kabla ya kufungwa kwa ziwa hilo upatikanaji wa samaki na dagaa ulianza kupungua kwa kasi na kusababisha wavuvi kutumia muda mrefu ziwani kusaka mazao hayo bila mafanikio, huku wakiambulia hasara.

Mchakataji wa dagaa mwalo wa Katonga, ziwa Tanganyika, Zena Masoud akizungumza na Mwananchi, anasema kabla ya ziwa hilo kufungwa bei ya dagaa wachache waliopatikana ziwani hapo walikuwa wakiuzwa Sh55,000 hadi Sh60,000 kwa kilogramu moja kutoka Sh10,000, lakini sasa ni kati ya Sh20,000 hadi Sh22,000.

Anaeleza kwamba ongezeko la bei hiyo ni kutokana na mitego ya kunasa dagaa na samaki kuongezeka ziwani hapo hivyo kuchangia uvuvi wa samaki na dagaa wachanga.

“Kwa mwaka jana kwa mwaka mzima nilichakata dagaa wasiozidi kilo 50, wakati miaka ya nyuma nilikuwa nachakata zaidi ya tani 10 kwa mwaka, siku chache baada ya ziwa kufunguliwa tayari nimeshachakata tani moja, kwa hiyo ilikuwa ni muhimu sana Serikali kuchukua hatua iliyochukua,” anasema.

Mwenyekiti wa wavuvi mwalo wa Kibirizi mkoani Kigoma, Paul Samwel anasema hatua ya Serikali kufunga ziwa Tanganyika imeleta matokeo chanya kwa wavuvi.

“Japo mara ya kwanza hatukukubaliana na ufungaji wa ziwa kwa sababu ndiyo shughuli yetu za kila siku, lakini kwa hali tunayoiona sasa baada ya ziwa kufunguliwa kidogo tunapata mazao mengi ya uvuvi, kwa wiki chache tangu kufunguliwa kwa ziwa wapo waliovuna hadi tani tatu,” anaeleza.

Anasema wanachopambania sasa ni kuboresha uvuvi na uhifadhi wa samaki ili kuvutia masoko ya kimataifa, kwani bado njia za kisasa zaidi zinahitajika kwa wavuvi na wachakataji kuboresha kazi zao.

“Wachakataji walikuwa wanaanika samaki na dagaa chini na tuliona ni kawaida, lakini tulipopewa mafunzo kupitia mradi wa FISH4ACP tuliona namna tunavyokosa masoko ya kimataifa na hata samaki na dagaa wanabeba vumbi na bakteria, kitendo ambacho hunyima fursa mazao hayo kupata masoko ya kimataifa,” anasema.

Samwel anasema matumizi ya umeme wa jua katika mahema maalumu ya kukausha samaki na majiko ya mkaa yameondoa changamoto ya dagaa na samaki kubeba vumbi na bakteria wakati wa ukaushaji.

Mradi alioutaja Mwenyekiti huyo unatekelezwa mkoani Kigoma, ukilenga kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi ziwa Tanganyika kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU), lakini utekelezaji wake unafanywa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri) mikoa ya Kigoma na Katavi.

Kaimu Ofisa Udhibiti Ubora, Viwango na Masoko Mkoa wa Kigoma, Theresia Malubya anasema kabla ya ziwa hilo kufungwa mazao yaliyopatikana hayakuwa na ubora.

“Mazao yaliyopatikana wakati huo yalikuwa madogo na hafifu, hata wachakataji walikuwa wakikosa mazao ya kuchakata kwa utimilifu na hata samaki na dagaa waliokuwa wakipatikana hawakuwa na ubora mzuri kwa ajili ya masoko tofauti,” anasema.

Mulubya anasema baada ya ziwa kufungwa na kufunguliwa aina ya dagaa na samaki wanaovuliwa wana viwango vinavyohitajika sokoni na tayari wamechukua sampuli za mazao hayo kupeleka maabara kuangalia muundo wa samaki dagaa na harufu.

Anasisitiza kuwa ni muhimu mradi wa FISH4ACP uendelee kugusa watu wengi zaidi, kwani kwenye sekta ya uvuvi wapo watu wengi wanaoingia kufanya shughuli hiyo bila kuwa na ujuzi wowote.

Mchakataji wa dagaa, Yohana Agustino  ndani ya hema maalumu la kukaushia dagaa kwa njia isiyoruhusu vumbi  wala bakteria ikiwa ni mbinu mpya inayotumika kukausha dagaa ziwa Tanganyika

Uuzaji dagaa nje washika hatamu

Kutokana na kuongezeka kwa ubora wa mazao ya uvuvi ndani ya ziwa Tanganyika, wasafirishaji wa mazao ya uvuvi ziwani hapo wameendelea kupata masoko ndani na nje ya nchi, ikiwemo Canada, Australia, Marekani, Uganda na Kenya, nchi ambazo walikuwa wakishindwa kuingiza mazao hayo kutokana na kukosa ubora.

Akizungumzia njia iliyotumika kuondoa changamoto ya wachakataji kukosa masoko nje, Mulubya anasema walipewa elimu kupitia mradi wa FISH4ACP kuongeza thamani mazao yao kuvutia masoko ya nje.

Yapo mafunzo wamepewa wachakataji, hasa kuhifadhi samaki kwa kutumia barafu na kuwaongezea thamani kabla ya kuwauza na wachakataji wengi wamekuwa na ujuzi huo na imesaidia kuongeza thamani mazao haya kusafirishwa nje ya nchi na sasa wanaelewa namna ya kuhifadhi mazao ya uvuvi kwa ajili ya biashara.

Kuanzia Juni 2023 hadi Julai 2024 samaki wabichi kutoka ziwa Tanganyika waliochakatwa na kuuzwa nchini Canada, Australia na Marekani, DR Congo, Zambia na Burundi ni jumla ya tani 66.9 kwa kuuzwa Sh43 milioni,” anasema Mulubya.

Mulubya, ambaye pia anasimamia ubora wa samaki mkoa wa Katavi na Rukwa, anasema samaki wakavu tani 174.5 walichakatwa na kusafirishwa nje na kuuzwa Sh88.5 milioni, dagaa wabichi tani 28.7 na waliingiza Sh22 milioni na dagaa wakavu tani 125.3 ambao waliuzwa kwa Sh90.9 milioni.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Usafirishaji wa samaki Mkuyu Fish Export iliyopo Kigoma, Jamilo Athumani anasema ubora wa mazao ya uvuvi ambayo hupata masoko nje ya nchi hutegemea aina ya ukusanyaji wake ziwani.

“Tumewapatia watu elimu ya namna ya kutukusanya dagaa na samaki na imetuwezesha kupokea mazao hayo yakiwa na ubora, tofauti na miaka ya nyuma tunaletewa bidhaa hizo tayari zimeshaharibika.

“Kinachofanyika tunawapa wavuvi barafu, wakienda kuvua wanahifadhi samaki na dagaa kwenye barafu na wanaopokea nao wanahifadhi kwenye barafu wanazifikisha kiwandani zikiwa na ubora,” anasema.

Athumani anasema kwa kuwa tayari wafanyabiashara wametengeneza masoko nje ya nchi, Serikali inapotaka kufunga ziwa kwa mara nyingine kwa makubaliano na nchi nyingine zilizopo mwambao wa ziwa Tanganyika ni muhimu ihakikishe makubaliano yao yanatekelezwa na kila mmoja.

Anasema wavuvi wa Tanzania wanapozuiliwa kuvua angali wapo wa mataifa mengine lilipo ziwa hilo wanaendelea kuvua, wateja hukimbilia maeneo hayo kupata mazao ya uvuvi ambayo huku Tanzania hayapo kutokana na ziwa kufungwa.

Anasema masoko ambayo Tanzania inayalisha samaki na dagaa wa ziwa Tanganyika ni Marekani, Canada, Australia, Kenya, Burundi na mataifa mengine ya Afrika.

Damian Remi, mmiliki wa Kampuni ya Ruhebeye inayojishugulisha na usafirishaji wa dagaa nje ya nchi kutoka mkoani Kigoma, yeye anasema baada ya ziwa hilo kufunguliwa tayari zaidi ya tani tatu za dagaa amesafirisha nje ya nchi.

“Sijawahi kusafirisha kiwango hiki cha dagaa nje ya nchi, pamoja na kwamba tulikuwa na dagaa wengi, lakini ubora nao ni mkubwa, sababu wachakataji kupitia mradi wa FISH4ACP wamejengewa uwezo wa namna ya kuongeza thamani mazao ya uvuvi,” anasema.

Kessy Amani, mvuvi mwalo wa Miyobozi wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma anasema baada ya kubaini wavuvi na wachakataji mmoja mmoja hawapewi mikopo na taasisi mbalimbali kutokana na shughuli zao kutotabirika, wameanzisha vikundi vya kutunza na kukopeshana fedha wenyewe kwa wenyewe.

“Hatukopeshwi kupitia kazi zetu mpaka upeleke hati ya nyumba, sasa wengine hizo nyumba hatuna, kwa hiyo tuliomba mikopo Serikalini kupitia halmashauri tumepatiwa boti na tupo wanakikundi 15, tukivua mazao yanauzwa fedha inawekwa kwenye kikundi mtu anakuja kukopa, akipata mtaji anarudisha anapewa mwingine,” anasema.

Anasema boti waliyokopeshwa ni ya Sh64 milioni na kila mwezi wanapaswa kurejesha Sh1 milioni, tayari tumeshatengeneza mitaji yao na makazi ya kuishi.

Amani anasema katika shughuli za uchakataji wa dagaa na samaki kazi kubwa hufanywa na akina mama na wanaume huingia kwenye kazi ya uvuvi, hivyo changamoto ya mitaji kwa wanawake wakati mwingine huwasukuma kuanzisha mahusiano na wavuvi ili wapate mazao, jambo ambalo ni hatari.

Naye Sia Kapela, mwanachama wa kikundi cha Kasi Mpya cha wachakataji mazao ya uvuvi anasema wameamua kujiunga kupitia vikundi ili wapate mikopo nafuu kwa haraka.

“Tunapokuwa kwenye vikundi ni rahisi kutambulika na kupata msaada, kwa hiyo tulianzisha vikundi kutatua kero zetu kwa kushirikiana na kuifikia Serikali kwa urahisi kuomba mitaji,” anasema.

Takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zinaonyesha kuwa kwa ujumla mavuno ya samaki nchini kuanzia Juni 2023 hadi Aprili 2024 ilikuwa tani 472,559 na tani 78,130 zilivunwa kutoka ziwa Tanganyika pekee.

Kwa mwaka 2024/25 Serikali kupitia bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi miongoni mwa vipaumbele vinavyotekelezwa kuinua sekta ya uvuvi ni kufanya mapitio ya Sera, Sheria na kanuni za sekta hiyo, kuimarisha taasisi za uvuvi ili kuongeza ushiriki katika uchumi wa buluu.

Pia Serikali inapanga kuimarisha uwezo wa uvuvi katika bahari kuu na kuongeza ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi, kuchochea uwekezaji katika miundombinu ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji na kudhibiti ubora wa mazao ya uvuvi na masoko.

Related Posts