Je, Mkuu wa sera za Kigeni ajae EU kuiunga mkono Israel – DW – 12.09.2024

Hata hivyo inaaminika kwamba atatafuta uungwaji mkono katika hatua za kuushughulikia mzozo wa Israel na Palestina.

Uteuzi wa waziri mkuu wa zamani wa Estonia, Kaja Kallas kama mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya, ulivuma kwa kiasi kikubwa huku Israeli ikipata afueni.

Magazeti ya Israel yaliangazia hasira za nchi hiyo dhidi ya mtangulizi wa Kallas, Josep Borrell, ambaye alielezewa kuwa mkosoaji wa wazi wa nchi hiyo, na kumsifu Kallas kuwa bora zaidi kwa mtazamo wa Israeli.

Daniel Schwammenthal, mkurugenzi wa Taasisi ya AJC Transatlantic, ofisi ya kamati ya Marekani na Kiyahudi yenye makao yake mjini Brussels, amesema Waisraeli wanamwona Borrell kama mkosoaji mbaya wa nchi yao na ambae hafai kuwa mpatanishi katika mzozo wa Israel na Palestina.

Soma pia:Mkuu wa sera za nje wa EU Joseph Borrell ashtushwa na mauaji ya mateka 6 wa Israel

Katika tathmini yake, Schwammenthal ameiambia DW kwamba, uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Israel unaweza kuboreshwa tu chini ya uongozi mpya.

Ukosoaji wa Borrell wa kampeni ya kijeshi ya Israeli huko Gaza tangu shambulio la kigaidi la Hamas la Oktoba 7, ulimweka katika msuguano na Israeli na kuonyesha mgawanyiko katika Umoja wa Ulaya juu ya mzozo huo wa Israeli na Palestina.

Austria, Ujerumani, Hungary na Jamhuri ya Czech zinaaminika kuiunga mkono zaidi Israeli  wakati Ireland, Ubelgiji na Uhispania anakotoka Borrell, zikiwa na ukosoaji zaidi.

Wanasiasa: Borreli aliegemea upande mmoja

Lukas Mandl, mbunge wa Austria katika Bunge la Ulaya, kutoka chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia cha European People’s – EPP, ameiambia DW kwamba anaamini Borrell aliegemea upande mmoja na kuwa na misimamo mikali kuhusu Israel. Mandl anatumai kwamba Kallas atakuwa bora kuliko mtangulizi wake.

 Brussel, Ubelgiji | Ursula von der Leyen akiwa na Kaja Kallas
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akiwa na Kaja KallasPicha: Geert Vanden Wijngaert/AP/dpa/picture alliance

Kwa mujibu wa wabunge wa Umoja wa Ulaya, wataalamu wa Estonia na mdau wa ndani wa Israel ambao DW ilizungumza nao, Kallas anatarajiwa kuchukua mtazamo wenye usawa na muongozo kutoka kwa nchi wanachama badala ya kujaribu kumiliki sera hiyo.

Umoja wa Ulaya unaunga mkono suluhisho la mataifa mawili kwa mzozo wa Israel na Palestina, kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Oslo.

Soma pia:Borrell: Vita vya Gaza ni “janga”

Mnamo mwezi Januari, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya walisisitiza msimamo huo kwa kauli moja.

Merili Arjakas, mtaalam wa Mashariki ya Kati na mtafiti katika Kituo cha Kimataifa cha Ulinzi na Usalama (ICDS), nchini Estonia, amesema jambo jema ni kwamba si Estonia wala Kallas aliye na msimamo mkali kuhusu maswali yasiyo ya Urusi na kwamba hii inamaanisha anaweza kujihusisha katika nafasi isiyoegemea upande wowote.

Hata hivyo, wanaamini kuwa atawezesha kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa katika Mashariki ya Kati kama anavyofanya huko Ulaya na kuishutumu Urusi kwa kuzivunja.

Mtazamo wa Israel kwa Kallas

Waisraeli wanatumai kuwa anaweza kuwa mshirika dhidi ya Iran, ambayo inaunga mkono makundi ya wanamgambo katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na Hamas, na ambayo pia imesambaza makombora kwa Urusi na kuihatarisha Ukraine na kwa kiasi kikubwa usalama wa Ulaya.

Kallas aliunga mkono haki ya Israeli ya kujilinda na kulishutumu kundi la Hamas, ambalo Umoja wa Ulaya umeliorodhesha kama kundi la kigaidi. Pia ameunga mkono suluhisho la mataifa mawili na kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano.

Evin Incir, mbunge wa Uswisi katika bunge la Umoja wa Ulaya anayegemea chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Socialsts and Democrats – S&D, anasema ana wasiwasi kwamba Kallas hadi sasa hajatoa kipaombele kwa hali ya kibinadamu katika ukanda wa Gaza na hasikiki kama vile kundi chama hicho cha S&D kinavyomtarajia kuwa.

Israel yazidisha mashambulizi katika ukanda wa Gaza

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Soma pia:Matamshi ya kiongozi wa Israel yakosolewa na nchi za Magharibi

Kinyume chake, Mika Aaltola, Mbunge wa Finnish katika chama cha EPP, alionyesha imani thabiti katika uwezo wa Kallas wa kufikia makubaliano.

Lakini sera yoyote ambayo hatimaye itakachukuliwa na Kallas kuelekea Israel, hakuna yeyote katika upande wowote wa mjadala wa Israel na Palestina katika Umoja wa Ulaya ana shaka lolote kwamba sera yake itaathiriwa na yeyote atakayeshinda katika uchaguzi nchini Marekani.

 

 

Related Posts