Kamati ya bunge yaipongeza wizara ya maji kwa ubunifu wa hatifungani ya Tanga uwasa.

Kamati ya Kudumu ya Bunge Maji na Mazingira ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Jackson Kiswaga imetoa pongezi kwa Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso na Menejimenti ta Wizara ya maji pamoja na kuimwagia sifa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (TANGA UWASA ) kwa ubunifu na uuzaji wa Hatifungani ya kijani ambayo imewezesha upatikanaji wa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 53.12 ambazo zinakwenda kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo ya Tanga Mjini, Mkinga, Muheza na Pangani.

Kamati ya Bunge imetoa pongezi hizo leo septemba 12 katika ziara ya hiyo Mkoani Tanga ambapo wametembelea na kukagua chanzo cha Maji cha Bwawa la Mabayani linalohudumia wananchi wa Jiji la Tanga na Wilaya za Jirani ambapo Kamati imefurahishwa na kuridhika na kazi ya utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa chanzo hicho cha maji, pamoja na kujionea miundombinu ya huduma katika eneo la Mtambo wa kutibu na kuzalisha maji wa Mowe ambapo pia ni eneo la utekelezaji wa mradi huo.

Awali akitoa taarifa fupi ya Mradi Mhe. Jumaa Aweso Waziri wa Maji amesema mpaka sasa wakandarasi tayari wamekwishapatikana ambao ni China Railway Co. ltd na STC construction Co. ltd, ambapo ni muda sasa wa kuanza rasmi kwa utekelezaji wa mradi huo ambao umelenga kuongeza uzalishaji wa maji kutoka Lita Milioni 45 mpaka Milioni 60 na unatarajiwa kukamilika mapema mwezi Oktoba, 2024.

Related Posts