Mitaala 96 Udsm yapitiwa upya iendane na wakati

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimefanya maboresho ya mitaala 96 kwa kuipitia upya ili iendane na soko la ajira.

Maboresho hayo yamefanywa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET) ambao unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na mitaala ya taasisi za elimu ya juu ili iendane na mahitaji ya soko la ajira pamoja na kuimarisha mfumo wa usimamizi wa elimu ya juu nchini.

Kupitia mradi huo unaodhaminiwa na Benki ya Dunia (WB), chuo hicho kimetengewa Dola za Marekani milioni 47.5 kuutekeleza kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2021 hadi 2026.

Akizungumza Septemba 10,2024 Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho (Mipango, Fedha na Utawala), Profesa Bernadeta Killian, amesema mitaala hiyo tayari imepitiwa na Wizara ya Elimu na sasa wataalam wanafanyia kazi maoni ya wadau kwa ajili ya kuidhinishwa na Seneti na kupelekwa Tume ya Vyuo Vikuu kuomba ithibati.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Mipango, Fedha na Utawala), Profesa Bernadeta Killian akizungumza wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo ilipofanya ziara kukagua utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET) katika chuo hicho.

Profesa Killian alikuwa akizungumza wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo ilipotembelea kukagua utekelezaji wa mradi wa HEET

“Katika zoezi hili wahitimu 8,000 na waajiri 4,000 nchini waliweza kutoa maoni yao juu ya uboreshwaji wa mitaala na waajiri wengi walisema bado wanatamani kupata wahitimu kutoka katika chuo chetu, ili tujenge uwezo wa wanafunzi wetu kukubalika katika soko la ajira lazima tukae vizuri kimiundombinu, tunaishukuru Serikali mradi wa HEET utaongeza ubora,” amesema Profesa Killian.

Kwa mujibu wa Profesa Killian, mradi huo unatekelezwa katika Kampasi Kuu ya Mwalimu Julius Nyerere Mlimani (MJNM), Taasisi ya Sayansi ya Bahari – Zanzibar na kuanzisha kampasi mpya kwenye Mikoa ya Lindi na Kagera.

Amesema pia kupitia mradi huo wamewajengea uwezo wanataaluma 10 ambao wamepelekwa kusoma nje ya nchi katika ngazi ya uzamili na 12 katika ngazi ya uzamivu na tayari watano wamehitimu masomo katika ngazi ya umahiri.

Amesema mradi umehamasisha wanafunzi wa kike zaidi ya 8,000 kutoka mikoa 15 ya Tanzania Bara na Zanzibar wasome masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko, akizungumza baada ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Waziri wa Elimu, Omary Kipanga.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko, amesema wanatamani kuona mradi huo unakamilika kwa wakati na unaanza kutoa huduma huku thamani ya fedha ikizingatiwa.

“Kazi ambazo zinafanyika kwenye vyuo ni nyingi, tunataka kila mradi uliopelekewa fedha utangazwe ili wananchi wajue kazi iliyofanywa na Serikali,” amesema Sekiboko.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo hicho, Mwanaidi Majaar, ameiihakikishia kamati hiyo kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati kama ulivyopangwa.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga, ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea katika vyuo mbalimbali nchini.

“Miradi imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika asasi za elimu nchini, lengo ni kuzalisha wanafunzi wenye sifa stahiki, ujuzi, maarifa na uzalendo kwa ajili ya maendeleo ya taifa,” amesema Kipanga.

Related Posts