WAMEYATIMBA. Ndicho unachoweza kusema kwa timu ya kikapu ya Savio baada kuingia katika mfumo wa wakali wa kuangusha mibuyu, timu ya Srelio, na kula kichapo cha pointi 65-53 katika mchezo mkali wa Ligi ya Kikapu Dar es Salaam (BD) uliofanyika kwenye Uwanja wa Donbosco, Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Srelio imejenga heshima ya kuwa ‘wazee wa dozi’ baada ya kuzichakaza mfululizo klabu kubwa kuanzia kwa Dar City iliyoipasua kwa pointi 78-75, Pazi kwa pointi 52-44 na Vijana ‘City Bulls’ kwa pointi 78-64.
Katika mchezo dhidi ya Savio, Srelio ilianza kuongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 23-16, na hadi kufikia mapumziko washindi walikuwa wanaongoza kwa pointi 49-46.
Hata hivyo, licha ya Savio kupoteza mchezo huo wachezaji wake Oscar Mwituka, Cornelius Mgaza, Sylivian Yunzu na Brian Mramba walionyesha kiwango kizuri.
Kwa upande wa timu ya Srelio, wachezaji waliowasha moto wa hatari walikuwa ni Spocian Ngoma, raia wa Zambia, Chary Kesseng wa Cameroon na Zadock Emmanuel, ambao walikonga nyoyo za mashabiki.
Akizungumza na Mwanaspoti kwenye Uwanja wa Donbosco Oysterbay, kocha msaidizi wa Srelio, Miyasi Nyamoko alisema kwa matokeo hayo wanaendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kucheza hatua ya 8-Bora.
“Hadi sasa tumebakiza mechi dhidi ya Crows na Mgulani (JKT), ambazo tunataka kushinda pia,” alisema Nyamoko.