Msako wenye mabucha wanaouza nyama ya punda

Kenya. Viongozi kaunti za Narok na Bomet nchini Kenya wamepanga kuanza operesheni za kukabiliana na wizi wa punda ulioshamiri, huku hofu ya nyama zinazouzwa katika mabucha kuwa ni ya punda ikizidi kutanda.

Viongozi hao wakiongozwa na makamishna wa kaunti zao, Kipkech Lotiatia wa Narok na Dk Omar Ahmed wa Bomet tayari wamekutana kupanga mikakati. Tovuti ya Taifa Leo ya nchini humo imeandika.

Timu hiyo itajumuisha maofisa kutoka idara ya mifugo, afya, huduma ya kitaifa ya polisi, maofisa wa utawala wa Serikali ya kitaifa (Ngao) na mfumo wa kilimo Kenya. Maofisa hao watafanya mikutano ya mara kwa mara kupanga mikakati ya kulinda wanyama wa kufugwa.

Lotiatia amesema timu hiyo itasaidia kusimamia sheria ya ulinzi wa wanyama na kuhakikisha nyama inayoliwa na wananchi imeidhinishwa na idara ya afya ya umma.

Aidha ameitaka timu hiyo kufanya ziara za kushtukiza katika bucha za kaunti hizo mbili na kuthibitisha ikiwa nyama inayouzwa kwa umma siyo nyama pori.

“Wale watakaonaswa wakiuza nyama katika maeneo yasiofaa au nyama ambayo haijaidhinishwa na idara ya afya ya umma watakamatwa na kufunguliwa mashtaka mara moja. Hii ndiyo njia pekee tutakayohakikisha kuwa wananchi wanakula nyama nzuri.”

Aidha amewaonya wananchi dhidi ya kuchinja na kula nyama ya wanyama waliokufa au walio wagonjwa kwani tabia hiyo inaweza kusababisha magonjwa na vifo.

Kwa upande wake, Dk Ahmed amesema wananchi wanapaswa kutoa taarifa juu ya watu wanaochinja mnyama aliyekufa ili hatua zichukuliwe mapema.

Related Posts