Naibu Waziri Sillo: Nchi imetulia na ipo shwari

Moshi. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo amethibitisha kuwa hali ya usalama nchini ni shwari na amelitaka Jeshi la Polisi kuimarisha mikakati ya usalama wa raia na mali zao kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Sillo ametoa kauli hiyo leo, Septemba 12, 2024, wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa maofisa wakuu waandamizi wa Jeshi la Polisi, uliofanyika katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS) Moshi, mkoani Kilimanjaro, sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya jeshi hilo.

“Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kulinda raia na mali zao. Nchi ipo shwari na tunatarajia uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani mwaka ujao,” amesema Sillo.

Pia ameongeza, “Ni matumaini yangu kuwa mkutano huu utasaidia kupanga mikakati ya kuimarisha usalama wakati wa uchaguzi ili wananchi waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura bila bugudha.”

Hivyo, amelitaka Jeshi la Polisi kuendelea kuimarisha maadili na nidhamu huku akisisitiza kuwa nidhamu ni msingi wa mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Ameelekeza pia kuweka mikakati ya kuimarisha usalama, kudhibiti ajali za barabarani, kuboresha mazingira ya polisi ngazi ya kata na kutekeleza mapendekezo ya haki jinai nchini.

“Niwaombe viongozi wa dini na jamii kuendeleza malezi bora kwa familia zetu kwa kufuata na kuzingatia mila na desturi za dini zetu, ili kuepusha mmomonyoko wa maadili unaoonekana kuwa chanzo kikubwa cha uhalifu nchini,” amesema naibu waziri huyo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camilius Wambura amethibitisha kuwa hali ya usalama nchini iko shwari na amewataka wananchi kutumia haki yao ya kidemokrasia kushiriki kwenye chaguzi zijazo.

“Ushwari huu unatokana na kazi nzuri wanayoifanya askari wetu pamoja na ushirikiano wa vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi,” amesema Wambura.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Ally Gugu amesisitiza kuwa wizara itaendelea kuratibu na kuwezesha majukumu ya polisi ili kuhakikisha jeshi hilo linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Related Posts