Saudi Arabia yarejesha tabasamu kwa watoto 30 wenye matatizo ya moyo

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Watoto 30 kutoka maeneo mbalimbali nchini wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) huku Sh milioni 700 zikiokolewa.

Upasuaji huo umefanywa kupitia kambi maalumu ya siku 10 ya uchunguzi na upasuaji wa moyo iliyofanywa kwa ushirikiano na JKCI na madaktari kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo Saudi Arabia.

Akizungumza leo Septemba 12,2024 wakati wa kuwaaga madaktari hao Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Tatizo Waane, amesema wagonjwa 50 wamefanyiwa uchunguzi na 30 wamefanyiwa upasuaji mkubwa.

“Tangu Saudi Arabia ianze utaratibu wa kuwaleta madaktari wake nchini imetumia Sh bilioni 4.5, upasuaji umekwenda vizuri na watoto wana afya njema, tunaishukuru Serikali kwa kuweka mazingira rafiki ya kukaribisha wageni,” amesema Dk. Waane.

Mmoja wa wazazi wa watoto waliofanyiwa upasuaji mkubwa, Esther Msangalawe, ameishukuru JKCI na madaktari hao kwa huduma hiyo ambayo imerejesha tabasamu kwa watoto wao.

Msangalawe ambaye ni mkazi wa jijini Mbeya, amesema mwanawe wa miaka mitano alikuwa na tundu kwenye moyo na mirija yake ya damu ilikuwa membamba na kwamba tatizo hilo liligundulika Juni mwaka huu.

“Mwanangu alikuwa anachoka na wakati mwingine anavimba, sikuwahi kujua kama ana tatizo hadi alipogundulika mwezi wa sita. Haikuwa rahisi lakini tunashukuru sana kwa msaada huu,” amesema Msangalawe.

Kwa upande wake Balozi wa Saudi Arabia nchini, Bin Ahmed Okeish, amesema mpaka sasa zaidi ya watoto 300 wamenufaika kupitia mpango huo.

Aidha amesema kupitia programu hiyo watu 6,898 katika nchi 169 duniani wamenufaika huku ikigharimu Dola za Marekani bilioni 108.

Related Posts