Leo Septemba 11, inatimia miaka 23 tangu lilipotekelezwa shambulizi kubwa la kigaidi duniani, Septemba 11, 2001, jijini New York, Marekani, tukio ambalo lilibadilisha sera za Marekani na uhusiano wake na mataifa mengine duniani.
Siku hiyo ya Jumanne asubuhi, magaidi 19 wa kikundi cha al-Qaeda waliteka nyara ndege nne za kibiashara za Marekani zilizokuwa zikielekea pwani ya magharibi mwa nchi hiyo na kuziangusha makusudi.
Ndege mbili za shirika la American Airlines; Flight 11 na United Airlines, Flight 175—zilitoka Boston ambapo ndege ya Flight 11 iligonga ghorofa la kaskazini katika Kituo cha Kimataifa cha Biashara (WTC) jijini New York City, saa 8:46 asubuhi. Dakika chache baadaye, ndege nyingine ya Flight 175 iligonga ghorofa jingine la kusini, saa 9:03 asubuhi, na kusababisha kulipuka kwa ndege hiyo na maghorofa yote miwili.
Ndege ya tatu, American Airlines Flight 77, iliyokuwa ikitoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles huko Virginia, ilianguka karibu na jengo la Pentagon saa 9:37 asubuhi na ndege ya mwisho, United Airlines Flight 93, iliyokuwa ikitoka Newark, New Jersey, ilianguka katika uwanja wa Shanksville, saa 10:03 asubuhi, baada ya abiria kuvamia chumba cha marubani na kujaribu kuwashinda watekaji nyara.
Katika muda wa chini ya dakika 90, ulimwengu ulibadilika. Takriban watu 3,000 walipoteza maisha siku hiyo na Marekani ikajikuta imetumbukia katika vita ambayo imekuwa ndefu zaidi katika historia yake, vita iliyogharimu takriban dola 8 trilioni.
Tukio la Septemba 11 siyo tu lilibadilisha mwitikio wa jumuiya ya kimataifa katika kukabiliana na ugaidi, lakini pia katika uhusiano wa mataifa mbalimbali. Marekani ilirekebisha sera zake za uhamiaji na kusababisha kuongezeka kwa utambuzi wa wageni.
Baada ya tukio hilo, Marekani ilianzisha operesheni maalumu nchini Afghanstan ili kukabiliana na vikundi vya kigaidi, kikiwemo cha Taliban. Baada ya miaka 20 ya operesheni yake nchini humo, Marekani iliondoa rasmi vikosi vyake mwaka 2021 baada ya Taliban kuingia madarakani.
Katika kipindi hicho cha miaka 23, Marekani ilifanikiwa kumuua kiongozi wa kikundi cha kigaidi cha al-Qaeda, Osama Bin Laden, mwaka 2011 akiwa katika maficho yake katika mji wa Abbottabad nchini Pakistan.
Pia, wamo watuhumiwa wanne wa shambulizi hilo ambao wanashikiliwa katika gereza la Guantanamo na kesi yao imekuwa ikipigwa danadana.
Wanazuoni wanazungumzia shambulizi la Septemba 11 kama kitovu cha mabadiliko ya uhusiano wa mataifa, hasa katika ushirikiano kwenye masuala ya ulinzi na usalama pamoja na mtazamo wa dunia katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea Dar es Salaam na Nairobi mwaka 1998, hayakutiliwa manani kwa sababu yalitokea katika nchi zinazoendelea, lakini lilipotokea Marekani kwenyewe, lilileta mtazamo mpya.
Anasema lilionyesha kwamba magaidi nao wana mbinu za hali ya juu kuliko ilivyotarajiwa, hivyo iliyasukuma mataifa kubadili mbinu za namna ya kukabiliana nao kupitia uhusiano wa kijeshi, kidiplomasia na kiuchumi.
“Sisi mataifa ya ulimwengu wa tatu tunafuata kinachoamriwa na wakubwa…hii imeleta mtazamo mpya kwamba kwa vyovyote vile, kuna baadhi ya mataifa hayataruhusiwa kuwa na nguvu, ndiyo maana tunaona walimuua Muamar Gaddaf kwa sababu ya kumdhibiti,” anasema.
Mwanazuoni huyo anaeleza kwamba baada ya shambulizi la Septemba 11, suala la usalama limekuwa ni ajenda kubwa kwa vyama vya Republican na Democrats inapofika wakati wa uchaguzi mkuu.
“Taifa lenye nguvu duniani, masuala ya ulinzi, uhusiano wa kimataifa, pamoja na kwamba imekuwa ni ajenda ya muda mrefu, lakini baada ya shambulizi hilo, imeleta aina mpya za siasa nchini humo, ni mgombea yupi anaweza kuhimili mikikimikiki ya dunia,” anasema.
Kuhusu Tanzania inavyoguswa na mabadiliko yaliyosababishwa na shambulizi hilo, Dk Loisulie anasema Tanzania inategemea misaada na mikopo kutoka mataifa makubwa kama Marekani, hivyo inapokea pia mashinikizo kutoka kwenye mataifa hayo.
“Kuna sheria na mikataba inatengenezwa kwa shinikizo la mataifa makubwa ambapo tunalazimika kukubaliana nayo ili kuendelea kulinda maslahi ya wakubwa,” anasema Dk Loisulie.
Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Salim Ahmed Salim, Denis Konga anasema tukio la Septemba 11 limeifundisha dunia kwamba hakuna nchi ambayo iko salama, hata kama ina nguvu kiuchumi au kijeshi kama Marekani.
“Ugaidi unapokuwa unaathiri maeneo mengine ya dunia, haimaanishi kwamba yale maeneo mengine yaliyoendelea, yenye teknolojia ya juu, hayawezi kuathiriwa kwa namna moja au nyingine. Kwa hiyo, hii ilibadilisha mtazamo kwamba inawezekana ukawa na bajeti kubwa, lakini bado ukaathiwa na ugaidi,” anaeleza.
Jambo jingine, anasema Marekani ilibadilisha sera zake za uhamiaji hasa katika kuingia na kutoka nchini humo. Anasema mataifa mengine pia yaliimarisha mifumo yao ya uhamiaji kuepuka madhara kama yaliyotokea Marekani.
Mwanazuoni huyo anabainisha kwamba tukio la Septemba 11 lilibadilisha fikra za dunia kwamba dunia haitawaliwi na nchi moja, hapo ndipo mataifa kama China, Russia na Umoja wa Ulaya (EU) zilianza kukunjua mbawa zao na kuchukua nafasi.
Konga anaeleza kwamba athari ya shambulizi hilo ni pamoja na mdororo wa kiuchumi uliotokea kuanzia mwaka 2006 hadi 2008. Anasema mdororo huo ulikuwa ni mwendelezo wa shambulizi hilo kwa sababu mataifa makubwa yalielekeza bajeti zao kwenye mambo ya ulinzi na usalama.
“Pesa nyingi zilikuwa zinatumika kwenye sekta za ulinzi na usalama, tukasahau sekta nyingine na sekta nyingine zikaendelea kufanya vitu vingine, kwa hiyo tukajikuta kwenye hali mbaya ya kiuchumi,” anafafanua mhadhiri huyo.