US, UK kutafakari ombi la Kyiv kulegeza vikwazo vya silaha – DW – 12.09.2024

Mataifa hayo mawili yameahidi kupitia kwa haraka maombi ya Ukraine kwao kulegeza vizuwizi  vya kushambulia ndani ya Urusi, huku yakiahidi msaada mpya wa kiasi cha dola bilioni 1.5 kuelekea msimu mgumu wa majira ya baridi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken na mwenzake wa Uingereza David Lammy, walionyesha mshikamano wakati wa ziara yao ya nadra mjini Kyiv, walikofika baada ya safari ya treni iliyodumu kwa masaa tisa kutoka Poland.

Ziara hiyo imejiri wakati wasiwasi unaongezeka kuhusu hali katika uwanja wa mapambano na mustakabali wa mashaka kuhusu msimamo wa Washington juu ya vita hivyo.

Waziri Blinken amesema atawasilisha mazungumzo yake na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kuhusu idhini ya kusmabulia ndani ya Urusi kwa Rais Joe Biden, na kuongeza kuwa Biden na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer watajadili suala hilo watakapokutana mjini Washington Ijumaa ya wiki hii.

“Nikizungumza kwa niaba ya Marekani, kuanzia siku ya kwanza, kama ulivyonisikia nikisema, tumerekebisha na kubadilika, kulingana na mabadiliko ya uwanja wa vita. Na sina shakama kwamba tutaendelea kufanya hivyo kadiri hali inavyobadilika,” alisema Blinken.

Ukraine | Blinken, Lammy na Sybiha mjini Kyiv
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andrii Sybiha wakiwa katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari katika Wizara ya Mambo ya Nje mjini Kyiv, Ukraine, Jumatano, Septemba 11, 2024.Picha: Mark Schiefelbein Pool via REUTERS

Uingereza yaahidi na mamia ya makombora

Madai ya Urusi kupata makombora mapya ya masafa mafupi kutoka Iran yanatishia kuimarisha zaidi nguvu ya Moscow kwenye vita, huku kukiwa na wasiwasi kwamba uchaguzi wa rais nchini Marekani unaweza kupelekea mabadiliko makubwa kwa mfadhili huyo mkuu wa Ukraine.

Blinken alisema Marekani itatoa kiasi cha dola milioni 717 katika msaada mpya wa kiuchumi kwa Ukraine – ambapo nusu yake kukarabati miundombinu ya umeme iliyoharibiwa vibaya na mashambulizi ya Urusi wakati ambapo msimu wa baridi ukikaribia.

Soma pia: Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Uingereza wawasili Kiev

Blinken amemshutumu Rais wa Urusi Vladmir Putin kwa kujiandaa kuutumia msimu wa baridi kama silaha dhidi ya watu wa Ukraine, na kusisitiza wakati akizungumza na waandishi habari kuwa msaada wao kwa taifa hilo hautafifia, na kwamba umoja wao hautavunjika.

Lammy kwa upande wake amekariri ahadi ya serikali yake ya chama cha Labour kutoka msaadawa kiuchumi wa pauni milioni 600, sawa na dola milioni 782 kwa Ukraine.

Uingereza, ambayo imekuwa ikishinikiza kulegeza vikwazo kwa matumizi ya silaha ya Ukraine, pia itatoa mamia ya makombora mapya ya ulinzi wa anga kwa Ukraine mwaka huu, aliongeza waziri Lammy.

Ukraine | Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy
Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza David Lammy na mwenzake wa Marekani Antony Blinken wakiwasili kituo cha treni mjini Kyiv. Jumatano Septemba 11, 2024.Picha: Mark Schiefelbein/picture alliance/AP

Urusi imekuwa ikisonga mbele kwenye mji muhimu wa Pokrovsk katika mkoa wa mashariki wa Donetsk, mwezi mmoja baada ya Kyiv kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza katika eneo la Kursk nchini Urusi.

Soma pia: Iran yaapa kuchukua hatua kujibu vikwazo vipya

Katika chapisho la mtandaoni Jumatano jioni, Rais Volodymyr Zelensky alibainisha kuwa alikuwa na mazungumzo “yenye tija” na Blinken na Lammy, na kuzishukura nchi zote mbili kwa msaada wao. Lakini aliongeza: “Ni muhimu kwamba hoja za Ukraine zinasikilizwa.

Hapo awali, Waziri wa Mambo ya Nje Andrii Sybiha aliwaambia waandishi wa habari: “Ni muhimu kuondoa vikwazo vyovyote vya matumizi ya silaha za Marekani na Uingereza dhidi ya malengo halali ya kijeshi nchini Urusi.”

Alipoulizwa jinsi Moscow itakavyojibu, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema jibu “litakuwa linalostahili”, bila kutoa maelezo makhsusi.

Chanzo: Mashirika

Related Posts