Mtwara. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za mauaji katika matukio mawili tofauti ambapo watuhumiwa hao, kila mmoja alitumia kipande cha mti kumshambulia mwenzake na kusababisha kifo chake.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Septemba 12, 2024, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mtaki Kurwijila amesema watu hao walipigwa na vipande vya mti, hivyo kujeruhiwa na kusababisha vifo vyao.
Amesema wanamshikilia Ally Abrahamu (43), mkazi wa Kijiji cha Mbangalambuyuni kilichopo Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara ambaye Agosti 22, 2024 alimshambulia mke wake, Catherine Chinave (69) akimtuhumu kumsaliti kwa kuwa na uhusiano na wanaume wengine.
Amesema Abrahamu alianza kumshambulia mke wake kwa maneno kisha akachukua kipande cha mti na kumpiga nacho wakiwa njiani kuelekea nyumbani, wakitokea kwenye kilabu cha pombe, wakati wa usiku na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda huyo ameeleza kuwa chanzo cha ugomvi huo ni mtuhumiwa kumlalamikia mke wake, Catherine kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na wanaume wengine, ndipo mzozo ukawa mkubwa baina yao.
Hata hivyo, inasemekana kuwa mtuhumiwa huyo alichukua kipande cha mti na kuanza kumshambulia, jambo lililomsababishia maumivu makubwa mwilini mwake na kusababisha kifo chake.
Kamanda huyo amesema mwanamke huyo alifariki dunia wakati anapelekwa hospitali na sasa mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi wakati upelelezi ukiendelea.
Katika tukio jingine, jeshi hilo linamshikilia Rashid Madogori (42), mkazi wa Kijiji cha Hiari kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, kwa kosa la kumuua mtu aliyefahamika kwa jina la Konde Boy, mkazi wa kijiji hicho.
Amesema tukio hilo lilitokea Septemba 4, 2024, saa 11 jioni ambapo ulitokea ugomvi baina ya mtuhumiwa na marehemu Konde Boy ambaye jina lake halisi halijafahamika, ambapo mtuhumiwa alichukua kipande cha mti na kumshambulia nacho sehemu za ubavuni na kusababisha kifo chake.
“Wafichueni wanaofanya uhalifu na mauji ili kujenga jamii iliyo bora, natoa wito kwa wananchi wa mkoa huu kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi wakati upelekezi wa matukio yote mawili bado unaendelea ambapo ukikamilika, watuhumiwa watafikishwa mahakamani,” amesema Kurwijila.
Kwa upande wake, Salum Issa, mkazi wa Mtwara mjini, amesema kuna haja ya kutoa tahadhari kwa watu ili waache kujichukulia sheria mkononi na kuacha kupigana.
“Unajua kupigana ni mambo ya kizamani, sasa hivi changamoto za kiafya ni kubwa, unaweza kumpiga mtu kibao tu akadondoka, akafa, ukaozea jela. Ni vema sisi wenyewe tukapeana tahadhari ili kujizuia na hasira ambazo zitatusaidia kuepuka hizo changamoto,” amesema Issa.