ZAIDI YA BILIONI 19 KUTEKELEZA MRADI WA UMEME VITONGOJINI MWANZA

MKUU wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya shilingi Bilioni 19 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Umeme kwenye vitongoji 135 Mkoani humo katika majimbo yote tisa.

Ametoa pongezi hizo leo Septemba 12, 2024 ofisini kwake wakati akizungumza na Ujumbe wa wakala wa Nishati Vijijini (REA) uliomtembelea wakiongozana na Cylex Engineering Company ambaye ndie mkandarasi wa mradi.

Amesema Mhe. Rais anaendelea kuboresha maisha ya wananchi wake kwa kasi ndio maana amemaliza kuweka huduma za umeme kwenye vijiji vyote nchini na sasa anaelekeza nguvu kwenye vitongoji kwa kuhakikisha wanapata Nishati Safi.

Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa Wakala kumsimamia Mkandarasi vema ili akamilishe mradi kwa wakati kwa mujibu wa mkataba ili kwa haraka huduma za umeme ziweze kuwafikia wananchi.

Vilevile, amemtaka mkandarasi huyo kutumia wananchi wazawa kwenye maeneo ya mradi katika ajira ndogondogo zitakazotolewa na kuhakikisha wanawalipa kwa wakati ili kuepusha migogoro isiyo lazima kwenye eneo la kazi.

Akizungumzia upatikanaji wa huduma ya umeme Mhe. Mtanda amesema Mwanza ina nishati ya kutosha kwani ni megawati 86 pekee zinatumika kwa sasa pamoja na kuzalishwa zaidi ya megawati 100 hivyo kumekua na ziada ambayo itatumika pindi miradi ya kimkakati itakapoanza.

Awali, Msimamizi wa miradi ya Wakala wa Nishati vijijini REA Kanda ya ziwa Mhandisi Ernest Makale amesema mradi huo kwenye vitongoji unadhihirisha na kubainisha nia ya serikali ya kuhakikisha kila kitongoji nchini kinakua na umeme ifikapo 2030.



Related Posts