KAMPENI YA TENDWE BUTIAMA KUPANDA MITI 6,000 – MWANAHARAKATI MZALENDO

Kampeni ya Tendwe Butiama, inayolenga kuhamasisha elimu, afya, na mazingira, inatarajiwa kuanza tarehe 26 Septemba na kufika Butiama ifikapo tarehe 13 Oktoba kwa ajili ya kushiriki kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambayo hufanyika kila tarehe 14 Oktoba.

Kampeni hiyo, ambayo inatekelezwa kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania, inalenga kuwafikia watu 1,000 kwa njia ya kambi za afya na shughuli za upandaji miti, huku ikihamasisha wananchi kuchangia madawati kwa shule za msingi ili kuboresha elimu. Meneja wa mahusiano na mawasiliano wa Vodacom Tanzania Zuweina Farah, alieleza kuwa kampeni hii ni sehemu ya kuenzi juhudi za Baba wa Taifa za kupinga umasikini, ujinga, na malazi duni.

“Kampeni hii, inayoadhimisha mwaka wa sita tangu kuanzishwa kwake, inalenga kuwahamasisha wananchi kushiriki katika kuboresha elimu na kutunza mazingira. Tumeweka utaratibu ambapo kila mtu atapanda miti kulingana na umri wake; kwa mfano, mtu mwenye miaka 30 atapanda miti 30”. Aidha, alibainisha kuwa kampeni hiyo pia inahimiza utunzaji wa afya kupitia matumizi ya baiskeli, kwani ni njia rahisi na bora ya usafiri kwa wengi.

Kwa mwaka huu, kampeni itatembelea mikoa 12, ambapo Vodacom inatarajia kukabidhi madawati 1,000, kupanda miti zaidi ya 6,000, na kuandaa kambi za afya kila watakapopita. Tayari washiriki zaidi ya 100 wamejiandikisha, na wananchi wote wanahimizwa kushiriki ili kuchangia maendeleo ya elimu na afya nchini.

Kampeni hii inatarajiwa kumalizika kwa kushiriki kwenye kumbukumbu ya Baba wa Taifa Butiama, ambako wananchi wataweza kushiriki katika shughuli za kijamii kama upandaji miti na kuchangia maboresho ya elimu na afya.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts