Kesi ya ‘waliotumwa na Afande’ kutajwa leo

Dodoma. Kesi ya jinai inayowakabili washtakiwa wa makosa ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam itatajwa leo kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma baada ya upande wa Jamhuri kukamilisha ushahidi.

Upande wa Jamhuri umeleta mashahidi 17 kwenye kesi hiyo namba 23476 ya mwaka 2024 inayowakabili washtakiwa wanne, ambao ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas maarufu Nyundo, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson (Machuche) na Amin Lema (Kindamba).

Kesi hiyo ambayo inasikilizwa mfululizo tangu washtakiwa walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 19, 2024, iko mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Zabibu Mpangule.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa faragha Agosti 20 na mpaka hadi Septemba 6 mwaka huu upande wa Jamhuri ulikuwa umekamilisha ushahidi, ukiwemo wa mtaalam wa Tehama kutoka Jeshi la Polisi na daktari aliyemtibu binti huyo.

Pia mahakama ilisikiliza ushahidi wa binti aliyefanyiwa vitendo hivyo, watu waliomsaidia baada ya kufanyiwa vitendo hivyo, wataalamu wa utambuzi na waliowachukua washtakiwa maelezo baada ya kukamatwa.

Wakili wa washtakiwa hao, Godfrey Wasonga amesema baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wake kesi hiyo itatajwa leo.

“Upande wa Jamhuri umeshafunga ushahidi wao kwa hiyo kesi itakuja mahakamani kwa ajili ya kutajwa leo Septemba 13, ambapo itapangiwa kusikilizwa Septemba 23 na kama washtakiwa watakutwa na kesi ya kujibu wataleta utetezi wao,” amesema Wasonga.

Related Posts