Kisukari na faida, hasara ya unywaji wa kahawa

Unywaji wa kahawa siyo jambo jipya kwa Watanzania, kuna hasara na faida za unywaji wake, hasa kwa wenye kisukari.

Faida za unywaji wa kahawa

Kinywaji hiki kina viambato kama vile polyphenols na antioxidants ambazo zinaweza kusaidia kuboresha mchakato wa insulini mwilini.

Hii ni muhimu kwa watu wenye kisukari kwa sababu insulini ni homoni inayosaidia katika usimamizi wa viwango vya sukari kwenye damu.

Kwa hivyo, kahawa inaweza kusaidia kupunguza upinzani wa insulin na kuboresha utendaji kazi wake.

Kahawa ina antioxidants, kama vile chlorogenic acid, ambazo zinaweza kusaidia kupunguza uharibifu wa seli mwilini.

Mara nyingi kama seli zikiharibika, huathiri upelekwaji wa insulin kwenye mishipa ya damu na inaweza kuwa na athari mbaya kwa watu wenye kisukari.

Kwa kuepusha hali hiyo, kahawa inaweza kusaidia kupungua au kuzuia uharibifu wa seli hizi mwilini.

Kahawa inaweza kusaidia kudhibiti uzito kwa sababu ya uwezo wake wa kuongeza kiwango cha kimetaboliki na kuboresha matumizi ya nishati.

Kwa watu wenye kisukari, kudhibiti uzito ni muhimu kwa sababu unene kupita kiasi unaweza kuathiri udhibiti wa sukari kwenye damu.

Kahawa yenyewe bila kuongeza sukari au viambato vingine vya kuongeza ladha, inaweza kusaidia katika kudhibiti hamu ya kula na kuongeza shughuli za mwili na pia kahawa haina wanga, angalizo wagonjwa wenye kisukari wasitumie kahawa kama dawa ya kupunguza uzito na wasiache kufanya mazoezi.

Kwa upande mwingine, unywaji wa kahawa kupita kiasi unaweza kulete athari kwa wenye kisukari, kunywa kahawa kwa kiasi kikubwa kunaweza kuhusisha na matatizo ya moyo, kama vile ongezeko la shinikizo la damu.

Hii ni muhimu kwa watu wenye kisukari, kwa sababu wana hatari kubwa ya kupata matatizo ya moyo na mishipa ya damu.

Kahawa ina cafeine inayoweza kuathiri viwango vya sukari kwenye damu kwa kuongeza uzalishaji wa homoni kama adrenalini.

Hii inaweza kuathiri uwezo wa mwili wa kutumia homoni ya insulini kwa ufanisi na hivyo kuongeza viwango vya sukari kwenye damu kwa baadhi ya watu.

Kusababisha mapigo ya moyo kuongezeka kwa baadhi ya wagonjwa wa kisukari, cafeine inaweza kusababisha mapigo ya moyo kuwa ya haraka au yasiyo ya kawaida.

Hii ni hali inayojulikana kama Arrhythmia na inaweza kuwa na athari mbaya kwa wale wenye matatizo ya moyo.

Cafeine yenye kahawa inaweza kuingiliana au kupunguza ufanyaji kazi wa dawa za kupunguza shinikizo la damu au dawa za kudhibiti mapigo ya moyo.

Hivyo, ni muhimu kwa watu wenye matatizo ya moyo kuzungumza na daktari wao kuhusu matumizi yao ya kahawa ili kuhakikisha kuwa haitaharibu matokeo ya matibabu yao.

Related Posts