Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za taasisi za kitaaluma za kimataifa zinazoonyesha dhamira ya kushirikiana na Zanzibar katika kuijengea uwezo wa kielimu katika nyanja mbalimbali.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Septemba 13, 2024 alipokutana na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Imperial cha Uingereza, Profesa Lam Wamsley na ujumbe wake Ikulu, Mtaa wa Laibon, Dar es Salaam.
Rais Mwinyi amesema bado nchi inahitaji kupanua wigo wa kitaaluma katika juhudi za kuleta maendeleo, kukuza uchumi na kuongeza maarifa na ujuzi wa watu wake.
Ameyataja maeneo ya biashara, afya, utafiti na teknolojia ya mawasiliano kuwa muhimu kwa nchi na yanahitajika kuendelezwa.
Rais Mwingi ameeleza kuunga mkono nia ya Chuo Kikuu cha Imperial cha Uingereza ya kufungua milango ya ushirikiano wa kitaaluma na kuanzisha programu tofauti kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza).
“Zanzibar imeendelea kuweka mkazo zaidi katika kuimarisha elimu ya juu ili kuandaa wataalamu katika sekta mbalimbali na bado inahitaji kuungwa mkono kimataifa,” amesema.
Ujumbe huo umekuja nchini kuangalia maeneo ya ushirikiano na hatimaye kuanzisha programu za mafunzo.