Namungo, Mgunda suala la muda

KOCHA msaidizi wa Taifa Stars, Juma Mgunda huenda kuna kitu kikatokea baina yake na Namungo, baada ya timu hiyo kurudi tena kuzungumza naye, ili kukinoa kikosi chao, tetesi zikisema ni suala la muda kumfuta kazi, Mwinyi Zahera.

Msimu uliopita, Zahera aliisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya sita, ikivuna pointi 36, ingawa alijiunga nayo katikati ya msimu akitokea Coastal Union ya Tanga, Ligi Kuu inayoendelea hajafanikiwa kupata matokeo.

Namungo imepoteza dhidi ya Tabora United (mabao 2-1), Singida Fountain Gates (mabao 2-0), Dodoma Jiji (bao 1-0), matokeo hayo yanaelezwa ndiyo sababu ya kuwa mtegoni kufukuzwa.

Japo alipotafutwa jana Katibu wa Namungo, Ally Seleman ili kuthibitisha hilo, alikana na kusisitiza jambo hilo sio kweli, kwa maelezo akili zao kwa sasa zipo kwenye mechi zilizopo mbele yao.

“Sifahamu kuhusu Mgunda, hadi sasa kocha ni Zahera, tunashirikiana ili kuhakikisha tunashinda mechi zilizopo mbele yetu, hilo ndilo jambo la msingi kwa sasa,” alisema Seleman.

Hata hivyo, chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa, Mgunda huenda akaungana na timu hiyo jijini Dar es Salaam na imefikia hotel ya Itumbi, iliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam, kilisisitiza mazungumzo ya viongozi na Mgunda yamefikia pazuri, hivyo kuna asilimia kubwa ya kufikia makubaliano hayo.

“Huenda Mgunda akaungana na timu Dar es Salaam, hiyo ndio taarifa ya awali niliyokuwa nayo, labda mambo yabadilike, kwani viongozi walikuwa wanazungumza naye na alionyesha utayari kwa asilimia kubwa,” chanzo hicho kilisema na kuongeza;

“Viongozi wa Namungo walipata nguvu ya kurudi kwa Mgunda, baada ya Simba kutangaza kuachana naye, baada ya kutumika timu ya wanaume na wanawake.”

Mgunda mwenyewe juzi wakati Stars ikirejea nchini alipoulizwa juu ya dili hilo la Namungo alijibu kwa ufupi;

“Ebu niacheni kwanza, nimechoka na safari.”

Related Posts