Patrick Aussems aanza kunogewa Bara

LICHA ya kuwa na mwanzo mzuri katika Ligi Kuu Bara, Singida Black Stars wanajua bado wana kazi kubwa mbele yao. Kocha wa timu hiyo, Patrick Aussems amesema licha ya kupata pointi tisa katika michezo mitatu iliyopita, anahitaji kuhakikisha kikosi chake kinakuwa bora zaidi.

Katika michezo mitatu iliyopita, Singida Black Stars ilivuna pointi sita ugenini baada ya kuifunga Kengold kwa mabao 3-1 na Kagera Sugar kwa mabao 1-0. Juzi, timu hiyo ilicheza nyumbani kwenye Uwanja wa Liti na kuendeleza wimbi la ushindi kwa kuifunga KMC kwa mabao 2-1.

Kocha Aussems aliwapongeza wachezaji wake kwa kiwango kizuri walichoonyesha, huku akiongeza walikuwa na nafasi ya kufunga mabao mengi zaidi hasa kipindi cha pili.

Alisema, “Tungeweza kuwa na mabao mengi zaidi kipindi cha pili, lakini tulishindwa kutumia vizuri nafasi ambazo tulitengeneza. Tunahitaji kuwa bora zaidi katika utumiaji nafasi, lakini mwishowe tumepata ushindi wa tatu mfululizo. Huu ni mwanzo mzuri kwa sisi.”

Aussems alisisitiza timu inaonyesha mabadiliko ya kiuchezaji na anaamini kuwa wataendelea kuboresha viwango vyao kadiri muda unavyosonga.

Kwa sasa, Singida Black Stars ndio wanaoongoza msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na pointi tisa, wakiwa wamefunga jumla ya mabao sita, sawa na wastani wa mabao mawili kwa kila mchezo, na wameruhusu nyavu zao kuguswa mara mbili, wastani wa 0.6.

Related Posts