Serikali kupitia REA yatenga Bilion 19 kusambaza umeme katika vitongoji 135 mkoani Mwanza

Serikali imezindua mradi wa kusambaza umeme wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 19 kwa ajili ya vitongoji 135 katika mkoa wa Mwanza. Mradi huo unasimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambapo Mhandisi Ernest Makale, amesisitiza umuhimu wa kufikisha nishati hiyo kwa wananchi wanaoishi maeneo ambayo hayajafikiwa. Hatua hii ni sehemu ya mpango mpana wa serikali wa kupanua upatikanaji wa umeme vijijini ili kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewataka wakandarasi wanaohusika na utekelezaji wa mradi huo kuhakikisha wanatoa ajira kwa vijana wa maeneo yanayohusika. Akisisitiza kuwa ni muhimu kwa wakandarasi kujali maslahi ya jamii kwa kuhakikisha kwamba vijana wanapata fursa za ajira kupitia mradi huo, jambo ambalo litasaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira.

Aidha, Mtanda aliongeza kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kwamba kila mwananchi anapata huduma ya umeme ili kuboresha ustawi wa maisha yao. Alieleza kuwa upatikanaji wa umeme ni nyenzo muhimu kwa maendeleo, kwani unawezesha upatikanaji wa huduma za afya, elimu, na kuongeza tija katika sekta mbalimbali za kiuchumi.

Mradi huu unatarajiwa kubadilisha maisha ya maelfu ya wananchi wa Mwanza, hasa wale wanaoishi maeneo ya vijijini. Kupitia mradi huu, serikali inatarajia kwamba upatikanaji wa umeme utaongeza fursa za kiuchumi, kupunguza umaskini, na kusaidia kufikia malengo ya maendeleo endelevu, hususan katika maeneo ya elimu, afya, na ukuaji wa viwanda vidogo vidogo.

 

Related Posts