Shuti la Fei Toto Lamtingisha kipa Simba

KIPA wa Simba, Moussa Camara ‘Spider’ alikuwa katika benchi wakati taifa lake la Guinea likiachia pointi tatu mbele ya Taifa Stars, lakini akaondoka na lile shuti la kiungo wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambalo lilizaa bao la kusawazishia kabla ya Mudathir Yahya kufunga la ushindi kwa Tanzania.

Fei Toto alifunga bao hilo kwa shuti kali la mbali lililomshinda kipa Ibrahim Kone aliyekuwa langoni likichomoa bao la utangulizi la wenyeji, kisha Camara kutamka kwamba ameshtuliwa na kiungo huyo anayekipiga Azam.

Camara ameliambia Mwanaspoti, Fei Toto aliwashangaza wengi kwa bao hilo ambalo liliwatibulia ambapo anataka kujipanga naye mapema kama atakuwa langoni watakapokutana na matajiri hao wa Chamazi.

Tangu atue Simba msimu huu, Camara ameanza katika mechi zote mbili za Ligi Kuu Bara sambamba na zile za kuwania Ngao ya Jamii, huku pia timu yake ikijiandaa kukutana na Azam ugenini Septemba 26.

Camara alisema bao ambalo Fei Toto amelifunga limemfanya kumfuatilia na kugundua mabao kama hayo ndio zake na amejipa kazi ya kuwa naye makini kila atakapokuwa anakutana naye hapa nchini kwenye mashindano.

“Unajua wote tulipokuwa kwenye benchi hatukutarajia kile kilichotokea, Feisal alifanya maamuzi ya haraka sana kutuliza mpira kisha kauchia shuti kali kila mmoja hakuamini pale nje,” alisema Camara na kuongeza;

“Kosa kubwa ambalo Kone alifanya ni hesabu zake ambalo hata mimi ningeweza kufanya lakini kwangu nimeiona nijiandae mapema na kitu kama kile kwa kuwa nitakutana naye hapo kwenye mashindano, sitaki kufanya makosa kama hayo.

“Niliangalia mabao yake nikaona pia anafunga sana kama hivyo kwa hiyo ukiwa kipa lazima ujiandae sana kujua unakutana na wachezaji wenye ubora gani.”

Septemba 26, mwaka huu ambapo ni siku chache baada ya Simba kumalizana na Al Ahli Tripoli katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika kuwania kutinga makundi, vijana hao wa Msimbazi watakwenda kukabiliana na Azam.

Simba na Azam zinakutana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo Camara mwenye uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza atakuwa na mtihani mbele ya Fei Toto.

Related Posts