Sikonge. Serikali imekumbushwa kutoa kibali cha ajira za watumishi katika Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora ili kukabiliana na upungufu wa watumishi 800 unaoikabili wilaya hiyo, hali inayozorotesha maendeleo. Wito huo umetolewa leo, Septemba 13, 2024, na Ofisa Mipango wa Wilaya ya Sikonge, Aidan Frument, wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge.
Frument amesema kada ya afya ni moja ya maeneo yenye upungufu mkubwa wa watumishi, ingawa wilaya hiyo imepunguza vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano kutoka 218 mwaka 2023/2024 hadi 154.
“Halmashauri yetu ina upungufu wa watumishi zaidi ya 800 katika kada mbalimbali, ikiwemo kada ya afya. Ukuaji wa watu katika halmashauri yetu ni mkubwa, na kwa kuwaajiri watu kwa mikataba na ajira za vibarua, hatuwezi kuwahudumia wananchi kikamilifu. Tunahitaji watumishi wa kudumu kwa ajili ya halmashauri yetu,” amesema Frument.
Hata hivyo, Katibu wa Afya wa Wilaya ya Sikonge, Suleiman Ally, amesema kwa mujibu wa ikama ya Ofisi ya Rais-Tamisemi, wilaya inahitaji watumishi 689 wa afya, lakini hadi sasa ina watumishi 274 tu, na hivyo kuna upungufu wa watumishi 424.
Ally ameeleza kuwa kada zinazokumbwa na upungufu ni pamoja na madaktari, wauguzi, wataalamu wa maabara, famasia, wataalamu wa radiolojia, na wataalamu wa mazoezi ya viungo.
“Kutokana na upungufu huu, zahanati moja inapaswa kuwa na watumishi 20, lakini sasa zahanati zina watumishi wawili au watatu tu. Hii ni hatari kwa sababu wanahudumia watu wengi, jambo linaloweza kusababisha huduma kutolewa chini ya ubora unaotakiwa,” amesema Ally.
Fatuma Cheya, mkazi wa Sikonge ameeleza hofu yake juu ya vifo vya watoto wachanga na watoto walio chini ya miaka mitano. Amesema wanawake wengi wanaogopa kubeba ujauzito kwa sababu ya vifo vinavyotokana na uhaba wa huduma za afya.
“Tunaiomba Serikali iongeze watumishi wa afya ili tuweze kupata huduma bora na watoto wetu wasipoteze maisha,” amesema Fatuma.
Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Colnel Maghembe amesisitiza kuwa licha ya kupungua kwa vifo, idadi ya vifo 154 bado ni kubwa na Serikali itaendelea kusimamia kada ya afya ili kuhakikisha idadi ya vifo inafikia sifuri.
Amesema vifo vya wanawake pia vimepungua kutoka 15 hadi 10, lakini juhudi zaidi zinahitajika.
Diwani wa Viti Maalumu wa Sikonge, Christina Samwel, amesema pamoja na mipango ya Serikali ya kuboresha huduma za afya, ni muhimu kuajiri watumishi zaidi ili kuondoa tatizo la kuzorota kwa huduma katika wilaya hiyo.