Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ameonya jana Alhamisi kuwa taasisi ya huduma ya afya ya taifa, NHS, inayofadhiliwa na serikali laazima ifanyiwe mageuzi au ife, baada ya ripoti huru kusema kuwa taasisi hiyo inayoheshimiwa iko katika “hali mbaya.”
Ripoti iliyowasilishwa na Lord Darzi, mtaalamu wa upasuaji na mwakilishi wa baraza la juu la bunge la Uingereza, iligundua kuwa NHS inakabiliwa na matatizo makubwa, mwenyewe akieleza kushtushwa na alichokigundua.
Akijibu ripoti hiyo, waziri mkuu Starmer aliahidi kuja na mpango wa miaka 10 wa marekebisho ya taasisi hiyo, ambayo katika miaka ya hivi karibuni imetoka kuwa chanzo cha fahari ya taifa hadi ishara ya serikali na jamii zinazokabiliwa na hali ngumu.
Soma pia: Chama cha Labour chaahidi neema Uingereza
Chama cha Starmer cha Labour kilipata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mwezi Julai, na waziri mkuu huyo amesema NHS inahitaji marekebisho makubwa ili kumudu gharama zinazoongezeka za kuhudumia jamii inayozeeka.