TFF, waamuzi wamlilia Abdulkadir | Mwanaspoti

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) na Chama cha Waamuzi wa Soka Tanzania (FRAT) wameonyesha masikitiko yao kutokana na kifo cha aliyekuwa mwamuzi mstaafu na mwenyekiti wa Frat, Omary Abdulkadir.

Abdulkadir aliyezikwa leo mchana katika makaburi ya Kisutu, alifariki dunia jana usiku kutokana na maradhi ya figo.

TFF imemwelezea Abdulkadir kama miongoni mwa watu waliotoa mchango mkubwa kwa soka la Tanzania.

“Rais wa TFF, Wallace Karia amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu (FRAT), Omary Abdurkadir.

“Ametuma salamu za pole kwa, familia, ndugu, jamaa, marafiki, FRAT, wanafamilia wa mpira wa miguu na wote walioguswa na msiba huo. Rais Karia amesema mchango wa Abdulkadir katika maendeleo ya mpira wa miguu kwenye eneo la waamuzi utakumbukwa daima.

Wakati wa uhai wake, Abdulkadir alikuwa mwamuzi wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kabla ya kustaafu, alikuwa mkufunzi wa waamuzi na mpaka mauti yanamkuta alikuwa mwenyekiti wa FRAT. Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi, Amina,” imesema taarifa hiyo ya TFF.

Taarifa ya FRAT imesema mchango wa Abdulkadir katika urefa wa soka hautosahaulika. “Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu FRAT, Emmanuel Chaula kwa masikitiko makubwa amepokea taarifa za msiba wa Mwenyekiti wa chama cha Waamuzi Omary Abdulkadir.

“Ametuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, waamuzi, wanafamilia wa mpira wa miguu na wote walioguswa na msiba huo.

“Abdurkadir alikuwa mwamuzi mstaafu wa FIFA na Mkufunzi wa Waamuzi Chaula amesema Abdurkadir alikuwa na mchango mkubwa sana katika maendeleo ya waamuzi wa Mpira wa Miguu hapa nchini. Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi, Ameen,” ilisema taarifa hiyo ya Frat.

Mtoto wa marehemu, Ahmed Omary alisema msiba huo umeacha pigo kubwa kwao. “Mzee alikuwa anaugua kwa muda mrefu maradhi ya figo. Kuna nyakati alipata changamoto kama vile presha lakini hasa kilichokuwa kinamsumbua ni figo. Sisi kama wanafamilia tumepata pigo kubwa sana maana mzee alikuwa ni mtu wa watu, mwenye upendo na muhimili.

“Hata hivyo, Mungu amempenda zaidi hatuna namna inabidi tukubali hili na tulipokee. Tunatoa shukrani zetu kwa wote walioshirikiana nasi kuanzia katika kumuuguza mzee wetu hadi sasa,” alisema mtoto huyo wa marehemu.

Abdulkadir anakumbukwa kwa kuwa refa wa pili wa Tanzania kuchezesha fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) ambapo alifanya hivyo mwaka 2000 wakati fainali hizo zilipofanyika Ghana na Nigeria. Katika fainali hizo, Abdulkadir alichezesha mechi moja tu ambayo ilikuwa ni ya hatua ya makundi ambayo Algeria ilipata ushindi wa mabao 3-1.

Katika mechi hiyo, Abdulkadir alimtoa kwa kadi nyekundu dakika za mwanzoni, mchezaji Eric Engo wa Gabon jambo ambalo lilikuwa gumzo.

Related Posts