Urusi yaishambulia Ukraine kwa droni usiku kucha – DW – 13.09.2024

Jeshi la anga la Ukraine limesema kuwa limezidungua droni 24 kati ya 26 zilizorushwa na Urusi usiku wa kuamkia leo katika mikoa yake minne. Wakati huo huo, Urusi nayo imeituhumu Jumuiya ya NATO kwamba inashiriki kufanya maamuzi katika jeshi la Ukraine. 

Katika taarifa iliyotolewa mapema leo katika mtandao wa Telegram, jeshi la anga la Ukraine limesema kwamba Urusi imeendeleza mashambulizi yake usiku kucha katika mikoa minne.

Soma zaidi. Je, NATO inapaswa kudungua droni za Urusi?

Kwa mujibu wa gavana wa mkoa wa Odesa, Oleh Kiper, ulioko kusini mwa Ukraine ni kwamba mabaki ya droni hizo yaliangukia katika eneo hilo na kujeruhi mtu mmoja na kuharibu nyumba 20 na makarakana manne.

Ukraine
Picha ikionyesha gari ya Ukraine ya msalaba mwekundu ikiwaka moto baada ya shambulizi la UrusiPicha: Police of the Donetsk Region via AP/picture alliance

Katika mkoa wa Mykolaiv, mashambulizi ya Urusi yalisababisha moto katika sehemu ya biashara ya chakula, hayo yamesemwa na Vitaly Kim, mkuu wa mkoa huo.

Wizara ya nishati ya Ukraine imesema Urusi ilifanya mashambulizi pia miundombinu ya nishati katika mikoa sita hapo jana na mkoa wa Ivano-Frankivsk ndio uliharibiwa zaidi ingawa hakukuwa na madhara zaidi katika shambulio hilo.

Urusi yaishutumu NATO

Katika hatua nyingine, Urusi imeishutumu Jumuiya ya kujihami ya NATO kuwa inahusika katika hatua ya kijeshi nchini Ukraine na kueleza kwamba inahusika katika kufanya maamuzi ya kijeshi.

Vyacheslav Volodin, mshirika wa karibu wa Rais  Vladimir Putin wa Urusi, na Mwenyekiti wa Bunge la Urusi ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Putin kutoa onyo kwa nchi za Magharibi kuwa zinaingia kwenye vita na Urusi moja kwa moja ikiwa zitaendelea kuruhusu Ukraine kuishambulia Urusi kwa makombora ya masafa marefu yaliyotengenezwa na nchi za Magharibi.

​​​​Vyacheslav Volodin
​​​​Vyacheslav Volodin, Mwenyekiti wa Bunge la Urusi ameitupia lawama NATO kuwa inashiriki katika maamuzi ya kijeshi nchinin UkrainePicha: Anton Novoderezhkin/ITAR-TASS/IMAGO

Akitoa maoni katika akaunti rasmi ya kituo cha habari cha Telegraph, Volodin ameongeza kusema kuwa Marekani, Ujerumani, Uingereza na Ufaransa kwa kujificha zinajadili kwa pamoja na Ukraine uwezekano wa kuishambulia Urusi kwa kutumia silaha za masafa marefu.

Soma zaidi. Urusi yaishambulia meli ya ngano na kuwauwa watu 3 Bahari nyeusi

Wakati vita hivyo vikiendelea kufukuta, Wizara ya mambo ya nje ya Romania imesema leo Ijumaa kuwa shambulio la Urusi dhidi ya meli ya nafaka ya Ukraine limechochea zaidi vita vyake dhidi ya Ukraine.

Ukraine iliishutumu Urusi siku ya Alhamisi kwa kutumia mbinu za kimkakati kushambulia meli ya nafaka katika shambulio la kombora huko katika Bahari Nyeusi iliyo karibu na Romania ambayo ni mwanachama wa NATO na kupelekea kuongezeka kwa mvutano baina ya Urusi na muungano wa kijeshi wa NATO.
 

Related Posts