WANANCHI WAISHUKURU SERIKALI KWA UJENZI WA DARAJA LA HOTOLWA..

NA WILLIUM PAUL, SAME.

WANANCHI wa kata ya Bwambo Jimbo la Same mashariki wilayani Same mkoani Kilimanjaro wameishukuru serikali kwa kuwajengea Daraja la Hotolwa linalounganisha kata hiyo na kata ya Mpinji.

Wakizungumza kwa hisia kubwa mbele ya Mbunge wa Jimbo hilo, Anne Kilango Malecela alipofika kujionea Daraja hilo na kisha kufanya mkutano wa hadhara walidai kuwa awali wamekuwa wakipata shida hasa kipindi cha mvua kutokana na kukosa kivuko cha kupita hali ambayo ilikuwa inapelekea kukata mawasiliano.

“Wapo ndugu zetu ambao wamefariki dunia kwa kusombwa na maji walipokuwa wakijaribu kuvuka kipindi cha mvua kutokana na kukosekana kwa Daraja lakini sasa kujengwa kwa Daraja hili ni furaha na neema kubwa kwetu sisi” Alisema Mariana Joseph mkazi wa kijiji cha Bwambo.

Naye Agustino Daniel alisema kuwa, watoto walikuwa wakikatisha masomo kipindi cha mvua mpaka maji yalikuwa yakipita katika eneo hilo yapungue ndipo wapite huku wagonjwa na wakinamama wajawazito wamekuwa wakiteseka kipindi wanapotaka kwenda hospitali.

Akizungumza na wananchi wa kata ya Bwambo, Mbunge Anne Kilango alisema kuwa, serikali imetumia zaidi ya milioni 196 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja hilo la Hotolwa lakini pia imetenga milioni 250 kwa ajili ya upanuzi wa barabara hiyo ya Bwambo – Ivuga yenye urefu wa kilomita 12.

“Serikali katika kuonyesha inawajali wananchi wa kata ya Bwambo na Jimbo la Same mashariki awali ilitoa milioni 250 kwa ajili ya kuichonga na kupanua barabara hii ya Bwambo – Ivuga pamoja na ujenzi wa Daraja hili lakini sasa barabara hii imetengewa fedha awamu ya pili milioni 250 kwa ajili ya kumalizia kazi zilizoanza kufanyika ili kuhakikisha inapitika muda wote” Alisema Mbunge Anne.

Alisema kuwa, daraja hilo ni muhimu katika kurahisisha mawasiliano ambapo barabara hiyo itarahisisha kufungua maendeleo ya wananchi wa kata ya Bwambo ambapo alisema kuwa kulikuwa na uhitaji mkubwa wa daraja kwani wananchi walikuwa wakiteseka kipindi cha mvua.




Related Posts