Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez amekutana na mgombea urais wa upinzani wa Venezuela Edmundo Gonzalez Urrutia, ambaye alikimbilia Madrid mwishoni mwa wiki akiomba hifadhi, huku mvutano ukiongezeka kati ya Caracas na mtawala wake wa zamani wa kikoloni.
Mkutano huo umekuja saa chache baada ya spika wa bunge la Venezuela kutoa wito wa kusitishwa uhusiano na Uhispania.
Soma pia:Mgombea urais wa upinzani Venezuela akimbilia Uhispania
Wito huo pia ulifuatia hatua ya wabunge wa Uhispania kupitishwa mswada usiofungamanisha kisheria, unaoitaka serikali ya Sanchez kumtambua Gonzalez Urrutia kama “mshindi halali” wa uchaguzi wa rais wa Julai uliompa Nicolas Maduro muhula wa tatu wa miaka sita.
Hapo jana Marekani ilitangaza vikwazo vipya dhidi ya maafisa 16 wa Venezuela, wakiwemo baadhi kutoka tume ya uchaguzi, kwa kuzuia “mchakato wa wazi wa uchaguzi” na kutochapisha matokeo “sahihi”.
Venezuela ilitoa taarifa muda mfupi baadaye na kushutumu vikwazo hivyo ikivitaja kuwa “uhalifu wa kichokozi”. Marekani pia imemtambua Gonzalez Urrutia kama mshindi halali wa uchaguzi huo.