Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kukosa umiliki wa viwanja, kutumia ndege kubwa kwa safari za ndani na bei ya nauli kuwa juu, zimetajwa kuwa sababu za shirika hilo kukosa ufanisi unaotarajiwa.
Imeelezwa fedha nyingi hutumika kwa shughuli za uendeshaji tofauti na mapato yanayopatikana.
Hayo yameelezwa wakati wa uzinduzi wa Kitabu cha ‘ATCL Business Model’ kilichoandikwa na Taasisi ya Media Brains, kikizungumzia namna shirika hilo linavyoweza kuongeza ufanisi katika utoaji huduma.
Kitabu hicho kinazinduliwa wakati ATCL kwa mujibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere hasara yake ilifikia Sh56.6 bilioni mwaka 2022/2023 sawa na ongezeko la asilimia 61 kutoka hasara ya Sh35.24 bilioni kwa mwaka uliotangulia.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Septemba 13, 2024, Mkurugenzi wa Taasisi ya Wajibu ambaye pia ni CAG mstaafu, Ludovick Utouh amesema ni wakati sasa kuacha kutumia ndege kubwa kwa safari za ndani, badala yake ufanyike uwekezaji katika ununuzi wa ndege ndogo zitakazokwenda mikoani, ili kupunguza hasara inayopatikana katika uendeshaji ikilinganishwa na mapato yanayopatikana.
Utouh amesema ripoti ya sasa ya CAG inaeleza utumiaji wa ndege kubwa kama Boeing 787 Dreamliner katika safari za ndani unaingiza hasara.
Akinukuu ripoti hiyo amesema kupitia safari hizo, ATCL iliingiza mapato ya jumla ya Sh45.67 bilioni na kutumia gharama za moja kwa moja za Sh70.57 bilioni.
“Hii ni sawa na hasara ya kiutendaji ya Sh24.9 bilioni. Tatizo hili linaweza kutatuliwa kwa kuongeza idadi ya ndege ndogo kwa safari za ndani na kuongeza idadi na miruko ya kimataifa kwa ndege kubwa,” amesema Utouh.
Akizungumzia umilikiwa wa viwanja, amesema ATCL kuendelea kulipia huduma mbalimbali katika viwanja vya ndege, imekuwa ikiongeza gharama za uendeshaji.
Utouh amesema ili kuondokana na hali hiyo, Serikali inaweza kuiga njia ya uendeshaji wa mashirika ya ndege kwa nchi ya Ethiopia kupitia Ethiopian Airways kwa kuachwa wawe huru na kufanya kazi kama taasisi ya biashara bila kuwapo mikono ya Serikali.
Amesema mfumo wa uendeshaji wa biashara wa Ethiopia Airways haujaruhusu shirika kujiendeaha pekee bali pia kuendesha huduma zote zinazohusiana na usafiri wa anga kama vile viwanja vya ndege, shule za mafunzo ya urubani na huduma za ardhini.
“Jambo hili linampa mtoa huduma wa ndege wa Ethiopia fursa ya kuzalisha mapato ya ziada na mapato ya kawaida ya ndege, pia inapunguza gharama za uendeshaji,” amesema Utouh.
“Serikali inachopaswa kufanya ni kuipa ATCL mazingira mazuri ya kujiendesha na kupunguza matumizi ya ndege hizo jambo ambalo linaipa mzigo na kuifanya kuingia katika hasara,”amesema
Akizungumzia nauli kuwa juu, Utouh ameshauri kuangaliwa namna ambayo nchi inaweza kujenga watu wa kipato cha kati ambao watakuwa na uwezo wa kutumia ndege pale wanapokuwa na shida.
“Kipato cha watu kinapopanuka na uwezo wao wa kununua tiketi unapanuka,” amesema.
Mkurugenzi wa Media Brains Tanzania, Jesse Kwayu amesema uwepo wa safari nyingi za ndege za ndani unaleta urahisi katika usafirishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.
“Baadhi ya watu tuliowahoji walisema zamani mtu wa Mpanda au Tabora alikuwa akitaka kwenda Dar es Salaam kwa ndege lazima aende Mwanza kwa basi ndiyo apande ndege, lakini hivi sasa ndege zipo zinazokwenda maeneo hayo,” amesema.
Kwayu amesema ndege inaleta nafuu katika usafirishaji lakini pia inafungua nchi; gharama ya nauli pekee ndiyo kitu kinachowaliza wengi.
Mmoja wa waandioshi, Neville Meena amesema kuifanya ATCL kuwa na huduma zote zinazohusiana na usafiri wa anga kama vile viwanja vya ndege, shule za mafunzo ya urubani, huduma za ardhini, kutachochea kupunguza gharama za nauli wanazotozwa wananchi.
Hata hivyo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa Mei 6, 2024 alisema ATCL imeanza hatua kwa hatua kujihudumia katika baadhi ya maeneo ikiwa ni pamoja na matengenezo ya ndege.
“Pia utoaji wa huduma uwanjani kwa kituo cha Dodoma, huduma ndani ya ndege na kutoa huduma ya mafunzo kwa wahudumu wa ndani ya ndege kupitia chuo chake cha ATCL Training Centre,” alisema.
Kwa mujibu wa kitabu cha hadithi za mafanikio ya ATCL katika miaka sita iliyopita kilichoandikwa na Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi, ATCL imeshuhudia ongezeko kubwa la idadi ya abiria wa ndani kutoka 32,000 hadi zaidi ya milioni moja hivi sasa.
Pia kumekuwa na ongezeko la ndege kutoka moja hadi 15, marubani 20 hadi 105 ambao asilimia 99 ni wa ndani.