NYOTA wa zamani wa Yanga na Coastal Union, anayekipiga kwa sasa Mashujaa, Crispin Ngushi juzi alifunga bao pekee lililoizamisha Coastal Union nyumbani na kuipa timu hiyo ushindi wa pili kitu alichodai kimempa mzuka akisisitiza kwa msimu huu kila mechi kwake ni fainali ili atimize lengo kurudi timu kubwa.
Ngushi, aliyesajiliwa na Mashujaa katika dirisha lililopita, alianza msimu na moto akionekana kama amefunga bao wakati timu hiyo ikiichapa Dodoma Jiji mjini Kigoma, lakini picha za marudio za Azam TV zilionyesha kipa Daniel Mgore alijifunga kwa krosi ya straika huyo kabla ya jana kumchambua kipa Ley Matampi wa Coastal wakati wakishinda kwenye Uwanja wa KMC, jijini Dar es Salaam na kuifanya timu hiyo ichupe hadi nafasi ya pili ikifikisha pointi saba baada ya mechi tatu.
Mashujaa ilitoka suluhu pia dhidi ya Tanzania Prisons na akizungumzia mwanzo mzuri wa timu hiyo na yeye mwenyewe, Ngushi alisema ni faraja na furaha kubwa kwao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ngushi alisema anafurahia maisha aliyonayo ndani ya Mashujaa na nafasi ya kucheza anayoipata kutokana na kuaminiwa na benchi la ufundi ataitumia kuhakikisha anafikia malengo.
“Yajayo siyafahamu ila nitatumia kila nafasi nitakayoipata kuhakikisha napata mafanikio yangu binafsi na kuipambania Mashujaa kufikia malengo suala la kucheza timu kubwa kila mchezaji ana ndoto hiyo, ikitokea nikarudi Yanga au kusajiliwa timu nyingine kubwa nitafurahi,” alisema Ngushi na kuongeza;
“Malengo ni kucheza kwa mafanikio bila kuangalia nani anafanya nini, kushinda mechi mbili tunaendelea kupata morali za kupambania pointi nyingine zaidi. Tunaelewa ugumu wa ligi lakini tutapambana kutumia nafasi tunazopata ili kujiweka kwenye mazingira mazuri.”
Alisema Mashujaa ina washambuliaji wengi na kila mmoja anatakiwa kutumia nafasi atakayopata kwa kufuata maelekezo wanayopewa na kocha kwenye uwanja wa mazoezi huku akikiri kuwa kwa upande wake anashindana na kivuli chake hashindani na mtu.
“Naheshimu uwezo wa wachezaji wenzangu nilionao kwenye timu moja na nipo tayari kutoa ushirikiano lengo likiwa ni moja tu kuipambania Mashujaa ifikie malengo na kwa upande wangu kuweza kuendelea kuwa kwenye ubora najivunia kupita kwa makocha wengi ambao kila mmoja amekuwa akiniweka kwenye ubora,” alisema nyota huyo wa zamani wa Mbeya Kwanza aliyoipandisha Ligi Kuu kabla ya haijashuka.