Benki ya CRDB yafanikisha uwekezaji wa Bilioni 790 kwenye uchimbaji wa grafiti Tanzania

Katika muendelezo wa jitihada zake za kuchangia ukuaji wa sekta za kimkakati na hatimae maendeleo ya nchi kwa ujumla, Benki ya CRDB leo imesaini makubaliano ya kuwezesha mradi mkubwa zaidi wa uchimbaji wa madini ya grafiti nchini Tanzania. Mkataba huo umesainiwa jijini Johannesburg nchini Afrika ya Kusini ambapo mradi huo chini ya kampuni ya Faru Graphite Corporation utagharimu Dola za Kimarekani Milioni 290 sawa na zaidi ya Bilioni 790 za Kitanzania.

 

Akizungumza wakati wa zoezi wa utiaji saini mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema “Tunajivunia kwa Benki yetu ya CRDB kupata imani hii ya wawekezaji wakubwa katika mradi huu ambao mbali na manufaa ya kibiashara kwa Benki lakini pia utakwenda kuchochea maendeleo ya maeneo ya Mahenge na Ulanga ambapo mradi huu utafanyika lakini pia utakua na mchango kwa Taifa zima kwa ujumla kupitia kodi zitakazolipwa pamoja na upatikanaji wa fedha za kigeni”

 

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Black Rock ambao ni wawekezaji wakuu kwenye kampuni ya Faru Graphite Corporation, John De Vries amesema kuwa wamefurahi kufanikisha hatua ya utiaji saini makubaliano na Benki ya CRDB ambayo imebeba jukumu la kusimamia uwekezaji wa fedha katika mradi huo.

 

Benki ya CRDB imebeba dhamana kubwa zaidi katika uwezeshaji wa mradi huo kwa kushirikiana na Benki za DBSA na IDC za nchini Afrika ya Kusini ampapo mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 26. Mbali na kampuni ya Black Rock inayomiliki kampuni ya Faru Graphite Corporation, Serikali ya Tanzania pia ina umiliki wa asilimia 16 katika kampuni hiyo kuendana na sera ya kushirikisha Serikali au kampuni za kizawa kwa uwekezaji kutoka nje.

 

Related Posts