Katika hatua muhimu ya kuendeleza juhudi za serikali za kuhakikisha kuwa raia wote wanapata bima ya afya, kampuni ya bima Tanzania ya Britam ilitoa bima ya afya bure katika hafla ya matembezi iliyoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania iitwayo Bima Walk iliyofanyika Dodoma.
Matembezi hayo yalikusanyisha wadau wa sekta ya bima na kutumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa kuwa na bima miongoni mwa Watanzania kwa kuongeza elimu ya bimu.
Britam ilimzawadia mshindi mmoja kutoka kwenye droo ya bahati nasibu iliyofanyika kwenye hafla hiyo, zawadi ya bure ya Bima ya Afya ya Afya Care kwa Samwel Joel. Mshindi alipewa kifurushi cha bima ya afya kinachotoa huduma za Matibabu ya Kulazwa (Inpatient) na Kutibiwa bila Kulazwa (Outpatient).
Mpango wa bima ya Afya Care ina vifurushi 12 vilivyoandaliwa kwa ajili ya mahitaji tofauti na vinatoa viwango mbalimbali vya faida.
Zawadi hii ni moja ya mpango wa kuendeleza juhudi na dhamira ya Britam ya kutoa suluhisho za bima za afya zinazopatikana kwa bei nafuu kwa Watanzania na inakamilisha juhudi za serikali za kueneza Sheria ya Afya kwa Wote.
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mheshimiwa Janeth Mayanja alisema, “Elimu ya bima inapaswa kuendelea kutolewa kwa umma.
Bima ni muhimu katika uthabiti wa uchumi wa nchi yetu na ustawi wa jamii. Kwa kuhakikisha kuwa raia wengi wanapata bima, tunalinda afya na ustawi wao wa kifedha.”
Dr. Baghayo Saqware, Kamishna wa Bima Tanzania alisema, “Maadhimisho ya tukio hili, itasaidia wananchi kuwa na imani na sekta ya bima na kutumia huduma mbalimbali za bima. Bima inadhumuni la kutoa kinga, na pia ni uwekezaji.”
Viongozi wote wawili waliipongeza kampuni za bima kwa juhudi za kuongeza uelewa wa umma kuhusu faida za bima, hususan bima ya afya, ambayo bado ni sehemu muhimu ya maendeleo ya kitaifa.
Bw. Farai Dogo, Mkurugenzi Mtendaji wa Britam Insurance, alitoa shukrani kwa washiriki na alisisitiza, “Tumejidhatiti katika kukuza thamani bora ya bima ya afya na kuhakikisha kuwa watu wengi wanapata huduma bora za afya.
Siku ya Bima inatoa fursa nzuri ya kuonyesha umuhimu wa bima ya afya katika kulinda ustawi wa kifedha na kimwili wa mtu. Kupitia droo hii, tunatumai kuleta athari chanya kwenye maisha ya mtu kwa kumpa zawadi ya utulivu wa akili na usalama wa kiafya.”
Jumamosi, tarehe 14 Septemba 2024, kampuni ya bima Tanzania ya Britam ilidhamini tukio la 27 la Siku ya Bima Tanzania lililofanyika Dodoma. Tukio hili lililenga kuangazia zaidi umuhimu wa bima katika kusaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania.
Kupitia mipango kama ‘Bima Walk’ na udhamini wa matukio muhimu ya sekta ya bima, Britam Insurance Tanzania inaendelea kuchukua nafasi ya uongozi katika kupanua upatikanaji wa bima ya afya na kuhakikisha kuwa Watanzania wengi wanapata bima, sambamba na malengo ya afya ya kitaifa.
Mgeni rasmi katika tukio hilo, Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalum, alisema, “Bima ya afya ni haki ya msingi ambayo inapaswa kupatikana kwa kila mwananchi. Serikali imejidhatiti kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanapata huduma za afya nafuu kupitia Sheria ya Afya kwa Wote, na tunapongeza juhudi za Britam Insurance katika kuunga mkono azma hii.
Mwitikio kama huu sio tu unawawezesha wananchi, bali pia unaleta nguvu katika mfumo wetu wa afya kwa kukuza ushirikishwaji na upatikanaji wa huduma kwa wote.”
Kuhusu Britam Insurance Tanzania:
Britam Insurance Tanzania ni kampuni inayoongoza kwa utoaji wa huduma za bima kutoa suluhisho za kibunifu na ya kina ya bima kwa watu binafsi na wafanyabiashara kwa kuzingatia ubora na kuridhika kwa wateja.
Britam Insurance Tanzania ilianzishwa mwaka 1998 na inatoa bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Bima ya Afya na Bima ya Jumla katika mikoa 6 nchini Tanzania ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha, Mtwara na Mbeya.