Buwasa yakabidhi mradi wa zaidi ya Bilioni 4 kwa mkandarasi huduma ya maji Bukoba kuboreshwa

Mamlaka ya Maji Safi na usafi wa mazingira Bukoba (BUWASA) imekabidhi mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji kwa ukanda wa juu kwa mkandarasi Daniel Lameck wa Kampuni ya Nice construction and general supplies limited ambao unatarajia kukamilika baada ya miezi 18

Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Bukoba (BUWASA) John Sirati amekabidhi mradi huo huku tukio hilo likishuhudiwa na Mkuu wa Wilaya Bukoba Erasto Sima ambaye alikuwa mgeni rasmi akiwa sambamba na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini Stephen Byabato,viongozi mbalimbali wa Chama na serikali pamoja na baadhi ya wananchi wa maeneo ya kata zitakazonufaika.

Sirati amesema kuwa mradi huo unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 4 na ukikamilika unatarajia kuongeza nguvu ya huduma ya maji na utahudumia kata 5 za manispaa ya Bukoba ambazo ni Rwamishenye,Kibeta,Kitendaguro,Ijuganyondo na Kagondo pamoja na kata mbili za Bukoba vijijin ambazo ni Kalabagaine na Katoma huku wananchi zaidi ya 55,000 wakitarajia kunufaika na mradi huo.

Aidha amesema kuwa mradi huo ukikamlika utamaliza changamoto ya maji katika maeneo hayo huku akieleza fursa ambazo wananchi watazipata ikiwemo kuwaunganishia bure huduma ya maji wananchi 2000 waliopo kwenye maeneo ya mradi huo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini Stephen Byabato amepongeza hatua ya serikali kuamua kuwaunganishia huduma ya maji bure wananchi 2000 huku akimuelekeza Mkandarasi wa mradi kutumia vijana wa maeneo husika pindi inapotokea fursa ya wao kushiriki kwa namna yoyote na sio kuwatoa nje ya eneo hilo sambamba na kuwataka vijana kutoa ushirikiano wa kutosha na kuwa waaminifu pindi watakapopewa kazi.

Pia mgeni rasmi ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Sima ameahidi kuusimamia mradi kwa umakini mkubwa kama miradi mingine huku akiwataka wananchi kuhakikisha wanatunza miundombinu katika mradi huo.

    

Related Posts