Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ametoa msisitizo kwa jamii za kitanzania kutumia utandawazi kuongeza maarifa katika kuleta maendeleo badala ya kuacha utandawazi uharibu utamaduni wa Taifa.
Mhe. Ndumbaro ametoa msisitizo huo wakati akifungua Mdahalo wa Kitaifa wa Maadili uliofanyika Septemba 14, 2024 katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ikiwa ni kuelekea Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa litakalofanyika kuanzia Septemba 20 – 23, 2024 katika uwanja wa Majimaji Songea.
Amesema Tanzania ina mila na desturi zake ambazo ni tofauti na mataifa mengine na kusisitiza kuwa wizara ina muongozo wa maadili katika shughuli za Utamaduni, Sanaa na Michezo ndani na nje ya Tanzania.
“Taifa lisilokuwa na Utamaduni wake ni mfu” haya ni maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Rais wetu wa sasa, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kutoa msisitizo kwa jamii kufuata mila na desturi za jamii ambapo kupitia maelekezo yake kwa wizara kuwa na Tamasha la Utamaduni kila mwaka kwa mikoa tofauti.
Ameongoza kuwa, utamaduni ndio msingi wa maadili pia ni mfumo wa uongozi, chakula, mavazi, elimu, sherehe, utamaduni usioshikika na unaoshikika.
Aidha, Mhe. Waziri ametoa wito kwa wana Ruvuma kujitokeza kwa wingi katika Tamasha hilo ambapo mgeni rasmi siku ya kilele Septemba 23, 2024, atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika hatua nyingine, amewasihi wananchi wa Ruvuma kujitokeza kujiandikisha na kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba mwaka huu.
Awali akimkaribisha Waziri, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni katika wizara hiyo, Bw. Boniface Kadili amesema Mdahalo huo ni sehemu ya utekekezaji wa Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 ambapo amesema sera hiyo inaeleza wajibu wa jamii katika kuenzi, kulinda na kukuza mila na desturi.