Arusha. Kukosekana mitaji, ardhi, na taarifa sahihi kunatajwa kuwa ni changamoto zinazowakabili vijana walio katika sekta ya kilimo.
Kutokana na changamoto hiyo, Serikali kwa kushirikana na wadau imeombwa kufanya mageuzi ya sera kuwawezesha vijana kuzalisha mazao ya biashara na chakula, kuongeza hali ya usalama na mifumo ya chakula kwa ujumla.
Hayo yameelezwa leo Jumamosi Septemba 14, 2024 na baadhi ya washiriki wa mjadala wa namna gani vijana na wanawake wanavyoweza kutumia fursa zilizopo kwenye mifumo ya chakula.
Kijana Magreth Malongo amesema baadhi yao wanakabiliana na changamoto hizo, hivyo kushindwa kufikia malengo ya kujikwamua kiuchumi na kuongeza uzalishaji katika kilimo.
Amesema fursa kwenye kilimo ziko nyingi lakini kuna wakati taarifa haziwafikii ili kushiriki kikamilifu.
Mbali ya hayo, amewataka vijana wenzake kulima kitaalamu na kutumia teknolojia ili kupata tija.
“Vijana si wote wanaopata elimu au mitaji, hivyo kwa kukosa elimu ya namna ya kufanya kilimo chenye tija na kutokuwa na uhakika wa masoko, kunachangia wengi kushindwa kukua kiuchumi kupitia sekta hiyo,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Sekta Binafsi la Kilimo (ANSAF), Honest Mseri amesema kwa kushirikiana na wadau wengine, wamekutana na vijana na wanawake kujadili mifumo ya chakula na namna wanavyoweza kutumia fursa zilizopo.
Amesema wanaangalia nini kifanyike nchini ili kuvutia vijana wengi katika kilimo kuhakikisha usalama wa chakula na lishe unaimarika.
“Tunafungamanisha sekta ya kilimo na afya kwani ili Taifa liweze kufanya mambo mengine yote muhimu yakiwemo ya maendeleo lazima liwe halina njaa, lina uhakika wa chakula. Watu wasipokuwa na utoshelevu wa chakula hata amani haitakuwepo,” amesema.
Amesema moja ya ajenda barani Afrika ni kumaliza umasikini, hivyo ni muhimu kama Taifa kuwa na mikakati kuwawezesha wakulima kujikwamua kwa kuongeza thamani kwenye kilimo wanachofanya kwa kutumia mbegu zenye ufanisi, mbinu bora za uzalishaji na masoko ya uhakika.
“Kwa sasa nchini kilimo kimeajiri watu wengi lakini mchango wake kwenye uchumi ni asilimia 25, lazima tuhakikishe watu waliopo kwenye sekta ya kilimo wanatoa mchango wa kutosha kwenye uchumi wetu,” amesema.