Dar es Salaam. Enzi zetu tulitatizika sana wakati tukitafuta wenza wa mbavu zetu. Hatukuwa na wepesi wa kuwafikia moja kwa moja maana watoto wa kike walichungwa sana. Pia hatukuwa na teknolojia ya kuwafikia kwa usiri kama simu za viganjani na barua pepe. Ilibidi kupiga hesabu za kuwinda paa hata kama hatukuwahi kuwinda mwituni.
Kulikuwa na tofauti kati ya mijini na vijijini. Vijijini hakukuwa na mambo mengi sana, familia zote zilifahamiana hivyo ilikuwa rahisi kwa waliotokana na familia korofi kukataliwa. Kijijini hakukuwa na longolongo. Yeyote aliyeamua kuingia kwenye mahusiano alijua kwamba hakuna majaribio wala kupimana. Wazazi walishirikishwa mapema na pengine hao ndiyo waliomchagulia kijana wao mwenza waliyemkubali.
Kijijini picha linaanzia kwenye uchochoro wa kutokea kisimani. Kijana anakwenda kutega nyuma ya mti jirani na kisima. Msichana anayemuota ni lazima angekuja hapo kuchota maji. Mara anamwona kwa mbali naye anachomoka mafichoni kuja kupishana naye.
Wanakutana katikati ya njia, kijana anasalimia kwa aibu na anajibiwa kwa aibu vilevile. Siku ya pili atapiga misele lakini safari hii ataongezea tabasamu la nusu mdomo. Macho yake yanayoibia kwa nyuzi arobaini na tano yanagundua tabasamu likijibiwa kwa aibu.
Kijana atakwenda kuandika barua ndefu ya kurasa mbili za katikati ya daftari. Anainakshi barua yake kwa viua vyekundu vikubwa na vidogo ili kuitia uzito. Atanyofoa kurasa na kuzificha mchagoni. Lakini hataiwasilisha barua hiyo kwa haraka, ataihariri mara kadhaa mpaka atakapojiridhisha kuwa imetimia. Baada ya subira ndefu ataukabidhi waraka huku akitetemeka mikono. Baada ya kubembeleza sana, atakwenda kusubiri jibu.
Binti atazingatia jinsi kijana anavyosumbuka juu yake. Pamoja na kuwaona mabinti wengine warembo kuliko yeye, lakini akaamua kuwekeza kwake tu. Na kwa vile jimbo bado halijachukuliwa, anakuwa radhi kumnong’oneza bibi au shangazi juu ya kijana yule.
Hilo ni jambo muhimu kuepuka majitu yanayokuja na maombi mikono ikiwa nyuma, lakini yakabadilika na kutunisha misuli mara baada ya kufanikiwa.
Huku mjini kulikuwa na shida kidogo. Watoto wa kike hawakwenda kisimani wala kukata kuni. Misele ilipigwa zaidi majumbani, kwani shuleni kulikuwa na hatari ya kunaswa na walimu. Mkinaswa huwa hamna utetezi, ni kichapo kwa kwenda mbele. Na kwa jinsi walimu wa nidhamu walivyokuwa na nongwa, wazazi wenu wangeitwa kuja kulaani na kutoa adhabu hadharani ili mkawe funzo kwa vicheche wenzenu.
Hivyo kwa asilimia nyingi kulikuwa na ulazima wa kubisha hodi kwenye milango ya sebuleni. Wazee walimwelewa kijana yeyote aliyekatiza uwani na kuzuga uhitaji wa chochote. Kama bahati yako mbaya utapokelewa na jibaba lenye ndevu hadi kifuani. Iwapo nyumbani hapo paliuzwa kashata au lawalawa ilikuwa rahisi. Vinginevyo ingekubidi uombe maji ya kunywa. Jibaba linakuletea kombe la bati lenye ujazo wa lita moja na kukukazia jicho vile unavyoyanywa.
Kwa kuwa lengo lako halikuwa maji, utarambaramba kona za kikombe na mzee atagundua nia yako. Atakupokonya kikombe na kukumwagia maji mgongoni pale utakapoanza kukimbia. Wale waliofanikiwa kupata miadi walikutana na misukosuko ya wajomba na mashemeji. Hata hivyo mwanaume alikaza buti na kuwa tayari kufa kuliko kumkosa mwanamke. Na hapo ndipo mtoto wa kike alipoongeza imani juu ya mvulana.
Watoto wa kileo wamerahihishiwa sana na teknolojia. Wanapekua statasi za mabinti kwenye mitandao ya kijamii na kutuma maombi kwa wasichana zaidi ya kumi. Mawasiliano na miadi huanzia humo. Lakini mara tu msichana na mvulana wakutanapo mubashara, wote wanagundua kuwa wamedanganyana. Mtoto aliiremba picha yake kwenye “snap” na kijana akajiongeza kwa “photo lab”. Imani inawapotea kabla mwendo hawajauanza.
Wadada huwa na njia nyingine. Mmoja anakosea namba kadhaa kwa makusudi na mara akutanapo na sauti za kiume, huanza na maswali ya “unafanya kazi gani”. Atazihifadhi namba hizo na kuendelea kuzisumbua ili kuwavutia wanaume kuwa anafikika. Wale watakaoonesha ushirikiano wataanza kupewa mahitaji kutokea chini kwenda juu. Kwanza hela ya bando, kisha hela ya kula. Baada ya muda mfupi atabainika uwezo wake wa kuhudumia marejesho ya mikopo.
Hii ni sababu mojawapo inayowafanya vijana kuyaogopa mahusiano. Utagundua kwamba wanaume wa sasa wanapenda kudeti na wadada walio tayari kwenye mahusiano. Kijana anaogopa kuingizwa kwenye mfumo wa kuhudumia “singo ledi” kwamba pengine yeye atakuwa mmoja kati ya makumi waliopangwa kwenye msururu wa msichana huyo.
Hali hii inaathiri pande zote. Kumbuka umri unakwenda bila kurudi, hivyo hufikia wakati mwanamke anakuwa na mahitaji na mwanaume (hata “mario”) kwa gharama yoyote. Ndiyo pale baba anayelea mabinti zake warembo anapogundua kuwa miaka imeenda na sasa analea wanawake.
Anabadilisha bango la “Tahadhari Mbwa Mkali” kuwa “Tunauza Ice Cream – Nyote Mnakaribishwa”.
Sina wazo la moja kwa moja ni nini kifanyike. Lakini wachunguzi waendelee kutafuta tamaduni zetu zilifanikiwaje, na wanaoiga tamaduni za ughaibuni wanafeli wapi.