Kilio cha haki za watoto chapelekwa kwa Bunge

Dar es Salaam. Wadau wa kutetea haki za watoto nchini wametoa wito kwa Bunge kufanya mapitio ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu kuwezesha kufutwa dhamana kwa makosa yote ya ubakaji na ulawiti kwa watoto.

Wito huo umetolewa leo Septemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam katika matembezi ya amani yaliyofanywa na wadau hao yakilenga kudai ulinzi wa watoto dhidi ya vitendo vya ukatili.

Akisoma tamko la wanamtandao wa kutetea haki za watoto kutoka Shirika la Wajiki, Janeth Mawinza amesema hatua hiyo itasaidia kuwaepusha waathirika kutishiwa na hata kuwekwa katika hatari ya kufanyiwa vitendo vingine vya ukatili.

“Tumekuwa tukishuhudia watuhumiwa wa makosa haya wakikamatwa na baada ya muda kutoroka au kuwa nje kwa dhamana, jambo ambalo husababisha waathirika kutishwa, kufanyiwa tena vitendo hivyo, kupoteza ushahidi,” amesema.

Amesema wanatoa wito kwa Jeshi la Polisi kuweka kipaumbele katika uchunguzi wa matukio ya aina hiyo na umma upewe taarifa sahihi na kwa wakati, pia ulinzi na usalama wa wananchi wakiwamo watoto uzidi kuimarishwa kuanzia katika ngazi ya kaya.

“Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutoa msisitizo kwa taasisi zote zenye dhamana ya ulinzi wa raia kutimiza majukumu yake na kukamilisha kwa haraka uchunguzi na mwenendo wa mashauri yaliyofikishwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ili haki itendeke kwa wakati,” amesema.

Mratibu wa wanawake watetezi wa haki za binadamu Tanzania, Hilda Dadu ametoa wito kwa jamii wakiwamo wazazi, walezi, walimu, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kuongeza ulinzi kwa watoto wakiwa nyumbani, kwenye taasisi za umma na binafsi, mtaani na mahali popote.

“Jamii inatakiwa kutambua umuhimu wa kushiriki katika ulinzi wa watoto hasa wenye ulemavu katika jamii yetu,” amesema.

Pia, ametaka wadau wa ulinzi na usalama wa mtoto kote nchini kushirikiana kumlinda mtoto ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii kuhusu ulinzi wa mtoto ikiwa ni pamoja na kuikumbusha Serikali kutimiza wajibu wake katika ngazi zote na kukemea vikali ukatili dhidi yao.

“Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha watoto wetu wanakua katika mazingira salama. Ni wakati wa kuchukua hatua madhubuti ili kuzuia matukio kama haya yasijirudie na kuhakikisha haki za watoto zinalindwa kikamilifu kwani ustawi wa watoto ni ustawi wa Taifa zima,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi amesema matukio ya ukatili kama kubakwa, kulawitiwa, kutekwa, na mauaji yamekuwa yanaongezeka.

Ametoa mfano katika Ripoti za Takwimu za Msingi za mwaka 2023 zinaonyesha ongezeko la matukio ya ubakaji na ulawiti.

Amesema ulawiti umeongezeka kutoka kesi 1,205 mwaka 2020 hadi 2,488 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 57 na ubakaji umeongezeka kutoka matukio 6,827 mwaka 2022 hadi 8,691 mwaka 2023.

Pia, amezungumzia matukio kadhaa ya hivi karibuni likiwemo la mtoto wa miezi sita kubakwa na kuuawa mkoani Dodoma, na mtoto wa miaka 13 kulawitiwa na kuuawa pamoja na mama yake.

Amesema vitendo hivyo ni kinyume cha haki za binadamu ambazo Tanzania imeridhia kuzitekeleza katika mikataba ya kikanda na kimataifa, ukiwemo Mkataba wa Kimataifa wa Haki ya Mtoto ambao katika ibara ya pili nchi wanachama zina wajibu wa kuhakikisha kunakuwa na mifumo itakayotoa ulinzi stahiki kwa mtoto bila ubaguzi.

Amesema katika mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto ambao pia Tanzania imeridhia, nchi wanachama katika ibara ya kwanza zina wajibu wa kuweka mifumo inayosimamia haki za watoto na kuhakikisha wanatoa ulinzi stahiki kwao na wanafurahia haki zao kama zilivyoainishwa.

“Wadau na watetezi wa haki za watoto tunalaani vikali vitendo vya kubakwa, kulawitiwa, kutekwa, kupotea, kuibwa na mauaji ya watoto vinavyoripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema.

Related Posts