KMKM yazindukia Mwembe Makumbi | Mwanaspoti

MABINGWA wa zamani wa Zanzibar, KMKM juzi jioni walizinduka katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu visiwani humo (ZPL) baada ya kuifumua Mwembe Makumbi City kwa mabao 2-1 baada ya awali kuanza ligi hiyo kwa kipigo kutoka kwa Mafunzo.

KMKM ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja na kuifanya ifikishe pointi tatu kama ilizonazo Mwembe Makumbi iliyopanda ligi hiyo msimu huu sambamba na Junguni, Tekeleza na Inter Zanzibar.

Bao la dakika ya 15 kutoka kwa Gaby Joseph na jingine la Enock Jiah dakika ya 50 yalitosha kuwazindua mabaharia hao wa KMKM katika ligi hiyo inayoingia raundi ya tatu sasa tangu ilipoanza Septemba 6, licha ya Mwembe Makumbi kupata bao la kufutia machozi katika dk23 lililofungwa na Yakub Said Mohammed.

Gaby alichaguliwa kuwa nyota wa mchezo na kuvuta Sh100,000 alizokabidhiwa papo hapo baada ya mechi hiyo iliyojaa ushindani.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo mmoja utakaozikutanisha timu zilizopo nafasi mbili za juu KVZ na Chipukizi kwenye uwanja huo huo wa New Amaan.

Chipukizi ndio inayoongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi nne kama ilizonazo KVZ ikitofautiana mabao, Chipukizi imefunga mawili kupitia michezo miwili, huku maafande wa KVZ wakiwa na moja ikiwa pia imecheza mechi mbili. Hata hivyo, timu hizo zilikuwa zinasikilizia matokeo ya mechi ya jana kati ya Zimamoto na watetezi wa ligi hiyo JKU ambayo kama imeshinda, ilikuwa na nafasi ya kuzitoa mahali zilipo.

JKU ilikuwa na pointi tatu na mabao matatu kabla ya mechi ya jana, hivyo ushindi au sare ulikuwa ukiifanya ikae kileleni wakati KVZ na Chipukizi zikishuka uwanjani leo.

Tofauti na msimu uliopita ligi hiyo ilipoanza na vipigo vikubwa na hat- trick katika mechi za mwanzoni tu, msimu huu mambo yamekuwa magumu kwani kabla ya mechi ya jana jioni, hakuna mchezaji yeyote aliyefunga bao zaidi ya moja, huku nyota watatu wa timu tofauti wakiwa wamejifunga na ushindi mkubwa zaidi ni wa 3-1 iliyopata JKU dhidi ya Inter Zanzibar na ule wa Uhamiaji ilipoikandika Junguni mechi za raundi ya kwanza.

Kesho Jumatatu kutakuwa na mechi mbili ukiwamo ule wa wageni Inter Zanzibar itakayoialika Malindi kwenye Uwanja wa Amaan B, Unguja, huku Kipanga na Junguni zikivaana Amaan A.

Related Posts