MaguRi, Makapu kuliamsha upya Biashara United

NYOTA wa zamani wa Simba na Yanga, Elias Maguri na Said Juma ‘Makapu’ ni miongoni mwa wachezaji wapya walioongeza mzuka ndani ya kikosi cha Biashara United kilichopo Ligi ya Championship inayoanza mwishoni mwa mwezi huu.

Nyota hao msimu uliopita walicheza katika timu za Ligi Kuu, Maguri akiwa Geita Gold iliyoshuka daraja, wakati Makapu alikuwa Mashujaa ambayo juzi iliifumua Coastal Union kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Biashara, Henry Mkanwa amesema uwepo wa wachezaji wenye uzoefu mkubwa ndani ya kikosi hicho, unampa ujasiri na urahisi wa maelekezo yake kufanyiwa kazi na kupata ushindi.

Biashara iliyokwama kupanda Ligi Mkuu msimu huu kwa kufungwa katika mechi za play-off na Tabora United, imetamba kiu yao ni kuona inasahihisha makocha kwa kukata tiketi ya Ligi Kuu msimu ujao.

Timu hiyo ya mkoani Mara itaanza msimu mpya wa Ligi ya Championship ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Karume, Musoma Septemba 22 dhidi ya Transit Camp kabla ya kuipokea pia Kiluvya United Septemba 28.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkanwa aliyeipandisha Tabora Utd, alisema anawajua mastaa hao vizuri kwani amewahi kuwafundisha wakiwa timu mbalimbali, hivyo, itamrahisishia kuweka maelewano mazuri na wachezaji chipukizi na kutengeneza muunganiko wa timu.

“Kupata wachezaji wazoefu kama Maguri na Makapu ni jambo zuri, hawa ni vijana ambao kwanza niliishi nao muda mrefu huko nyuma kwahiyo wananielewa na kufuata maelekezo yangu na kuyapokea,” alisema Mkanwa na kuongeza;

“Hii ni faida kwa wachezaji chipukizi watasaidia kujenga uhusiano mzuri kwenye timu, kwahiyo hawana shida hawa wachezaji wakubwa, wako vizuri wanaheshimu na kuelewa kile ambacho mwalimu anafanya.”

Kuhusu maandalizi ya timu hiyo, Mkanwa alisema yanakwenda vizuri na vijana wake wako tayari.

Related Posts